Barua Kwa Raisi Kikwete Toka Kwa WANANCHI TARAFA YA NYANJA MAJITA MUSOMA VIJIJINI

Barua Kwa Raisi Toka Kwa WANANCHI TARAFA YA NYANJA MAJITA MUSOMA VIJIJINI

Kilio Chetu Kwako Mh Rais Wa Jamhuri Ya Muungano Wa Tanzania Jakaya Mrisho Kikwete.

Sisi wananchi wa Musoma Vijijini Tarafa ya Njanja Majita tunapenda
kuleta kilio chetu kwako Mh. Rais tuliyekupigia kura wakati uchaguzi
uliopita na ambaye tutakupigia kura uchaguzi ujao 2010 ili uweze
kumaliza kipindi chako cha miaka Kumi katika madaraka.Tunakuomba usome waraka huu vizuri kasha utujibu sisi wananchi hata kupitia vyombo vya habari,hatutaki Mbunge wetu aje aseme kwa niaba yako kwani si mpenda maendeleo hasa huku Majita.

Tarafa ya Nyanja ina Kata 12 ,na kila kata kuna shule zaidi ya
moja,Tarafa hii inasifika sana kwa uvuvi wa samaki na dagaa hasa kule
Busekera,na baadhi ya vitiongoji vilivyopo kando kando ya ziwa .
Wananchi tunachangia kulipa kodi ya serikali kama itavyotakiwa
japokuwa hatujawahi kuambiwa ni kiasi gani cha kodi tumechangia katika mwaka wa fedha.

Tarafa yetu hii imekuwa na matatizo mengi sana na sugu ambayo
yametufanya tuachwe nyuma kimaendeleo ukilinganisha na upande wa pili wa musoma vijijini nazungumzia Butiama na vitongoji vyake . Nadhani hata wewe Mheshimiwa Rais ulipokuja kwenye Mkutano Mkuu wa Halmashauri ya Taifa miezi michahche iliyopita ulipata fursa ya kuonyeshwa maendeleo ya huo upande hasa kujengwa kwa shule za kisasa ambazo baadhi zao kuna Computer na madawati lakini kwa bahati mbaya Mbunge wetu hakuchukua jukumu la kukuleta wewe au mawaziri wengine katika tarafa yetu ili waone nini amefanya,huku majita hakuna kabisa alichofanya zaidi ya kutoa misaada ya mabati na genereta ambayo nayo ipo hapo takribani miaka mitano na itaoza.

Matizo tuliyo nayo sisi wananchi ni mengi ambayo Mbunge wetu
hameshindwa kuyatatua kabisa na kuegemea upande mmoja wa kwao.
Naomba nianzie upande wa shule za Msingi kwa ujumla shule si nzuri na hazipo kwenye hali ya kuridhisha kabisa ,wanafunzi wanakaa nchi
kutokana na ukoisefu wa madawati ,vyoo hakuna ,na isitoshe hata kama vyoo vipo basi vimejaa tayari Kwahiyo ,watoto wetu wanakuwa kwenye hatari ya kupata maambukizo kutokana na kutokuwepo na vyoo safi .Mbali na hilo shule hazina madawati ya kutosha ambapo wanafunzi wanakaa kwenye mawe kama enzi ya Mkoloni.Walimu pia hakuna kabisa,mtoto anamaliza shule hafahamu hata kuandika au kuongea kiingereza sababu kubwa wanadai uhaba wa walimu ,vifaa vya kufundishia hakuna kabisa japokuwa tunalipa kodi zetu kwa Serikali ili tuweze kunufaika kodi yetu.Kwa kweli Mh Rais kama kuondoa ujinga katika tarafa yetu hii itakuwa ni historia.Tunasikia kwenye radio kuwa kumetokea ubadilifu wa pesa za ualimu,Serikali inawasomi kwani wasitatufe njia ya kufatilia ni walimu wangapi wamelipoti kazini na pia kuwe na unique namba za ku track record za walimu.

Sekondari zipo 15 katika tarafa ya njanja ,tatizo ni uhaba wa ualimu
hakuna ,vifaa hakuna vya kufundishia wanafunzi,mahabara kw ajili ya
kufanya practical hakuna kabisa,watoto tunawalipia karo kila mwaka
lakini inapofikia wakati wa kumaliza shule na matokeo yakitotoka ni
zero ndiyo nyingi na wachache tu hawafiki hata 20 ndiyo wanachaguliwa kuendelea na kidato cha tano.Ili tatizo limekuwa sugu nenda rudi lakini hakuna uvumbuzi wowote ule,tumejaribu kumwambia Mbunge wetu amekuwa ni Mbunge wa kuturidhisha na vijibati vichache huku akiegemea kwake tu.Zaidi la hilo walimu hawaingii darasani kabisa na wanalipwa mishahara mwisho wa mwezi,kumbuka pesa ya mshahara niya walipa kodi.Inaumiza kama mlipa kodi hapewi huduma ya kuridhisha.Kadhalika amekuwa akijenga shule huko kwao tu na kupeleka wafadhili kuona maendeleo je huku majita hapaoni?na kama wafadhili wanatoa misaada je wanatoa kwao?Rais tusaidie ili na sisi Majita tuendelee.

Hospitali ambayo ndiyo huduma muhimu hapa katika tarafa yetu ya
Nyanja,cha kushangaza tuna dhahanati moja tu ya Mrangi ambayo
imekuwepo hapa tangu enzi ya Mkoloni hadi leo na haijawahi kufanyiwa
marekebisho ya haina yoyote yale wa upanuzi,Kweli Mh Rais fikiria
tu,tangu enzi ya Mkoloni idadi ya watu itabakia kuwa ile ile?Hapana
idadi ya watu imeongezeka sana kwa hiyo dhahanati hii ni ndogo sana na haiwezi kukidhi huduma kwa jamii kwa hiyo tunaishia kupoteza
watu,Mbali na hilo wakina mama wajawazito wanakufa sana hasa wakati wa kujifungua,sababu kubwa ni ukosekanaji wa wakunga na vifaa au wakunga hawapati mafunzo ya kutosha na siyo tu wakina mama pia watoto wetu wanafariki kila kukicha kutoka na kutokuwa na Zahanati nzuri na kubwa yenye huduma bora zikiwemo na madawa, Zahanati yetu hii wakati wote haina madawa kabisa.Mbali na watoto kuna magonjwa mengine yanatumaliza bila sisi wenyewe kufahamu mfano,Kisukari,Ugonjwa wa Moyo,Shinikizo la damu, Malaria , Transmission disease. Kisa hakuna waganga,ma nurse, mahabara, madawa, pia choo hazilidhishi kabisa.Kwa kifupi hudumu hakuna kabisa wakina mama,watoto,wazee wanakufa kila kukicha,kwa wale walio na ndugu wenye uwezo ndiyo watasafirishwa kwenda Musoma Hospital
kutibiwa japokuw ana yenyewe mpaka ufahamiane na mtu.

Huduma ya Maji hakuna kabisa ,bado wananchi wanasafiri mile 10 kwenda kuteka maji ili aje atoe huduma nyumbani,Kweli serikali inashindwa kupata wafadhili wa kusambaza maji majita wakati ziwa lipo?Kama Musoma mjini wamepata wafadhili kutoka Ufaransa na wemetoa kiasi cha bilioni 14 ,je sisi tunashindwa nini?Mbunge anafanya kazi gani?Yeye ni kwao tu ,tumechoka Rais na Mh Mkono. Sisi wazee tunakuomba baba utuletee mfadhili wa kusambaza maji safi.Mpaka tunazeeka hatujawahi kuona bomba japokuwa enzi za mkoloni kulikuwapo na bomba.

Barabara bado ni mbovu sana hasa ukizingatia tunatoa huduma ya uvuvi wa samaki huku ,wakati mvua zikinyesha inakuwa shida kubwa sana. Kwa ujumla barabara ni mbovu sana,kwa hiyo tunahitaji lami kama itawezekana Hatufahamu serikali inatoa kiasi gani cha pesa hasa katika tarafa yetu hii,sisi hatujui kabisa,tunasemewa na viongozi tu ambao hata kufika huku hakuna,report unayopewa niya uongo kwa wakandarasi hawajawahi kufika huku kujionea taabu tunazopata..

Umeme hakuna japokuwa ,tunasikia kwenye vyombo vya habari ya kuwa serikali ya Marekani ilitoa pesa kwa ajili ya kusambaza umeme vijijini lakini na kama ni kweli sisi wananchi hatupati taarifa kabisa hata Mh Mkono hasemi chochote.Hayo ni baadhi ya huduma kwa jamii ambayo kwayo sisi wananchi wa Majita hatupati na hatufahamu tunapata fedha kiasi gani katika bajeti.

Mh. Rais unaweza kutuuliza swali sisi wananchi kwanini hatujapeleka
haya malalamiko kwa Mbunge wetu ili yeye aweze kuyafikisha kwenye
vyombo husika vya Bunge?,Jibu ni kwamba Mbunge wetu ni shida sana
kumpata ,pia anatudharau sisi wananchi kwa sabau hatujui kitu na
hatujasoma ni kweli hatujaenda shule lakini ni vyema atusikilize sisi
lakini cha ajabu ,anadiriki kusema kwetu kwenye ubunge hawezi kutoka
kabisa hata msiponipigia kura ,anadai ataununua ubunge kwa gharama ya aina yoyote ile ili kwamba aendelee kubakia madarakani.

Hii inamaanisha kuwa rushwa itatolewa kwa wananchi hasa kwa wale
watakao rubunika ili kwamba wampigie kura mwakani aendelee kubakia
Mbunge.Mbunge wetu anadiriki kudharau hata baadhi ya viongozi wa kata na Wilaya kwa sababu ya pesa aliyo nayo na kuleta mabati tu,na kutoa vijisenti kwa mfano alileta generator kwenye sekondari miaka mitano iliyopita baada ya muda akaleta simtank la lita 1000 kutokea hapo hakuna kitu chochote kile ,sisi kama wananchi hatuna uwezo. Japokuwa vyote vipo hapo havifanyi kazi anasubiri uchaguzi ufike amwage pesa,khanga na vitenge ili achaguliwe tena.RUSWA AU TAKRIMA

Mh Rais sisi wananchi hatuelewi tunachangia kiasi gani kwenye kodi , na pia hatujui inatumika vipi,mbali na hilo serikali inatoa pesa kwakila
wilaya lakini sisi tukimwuliza Mbunge wetu hatuambii kitu chochote
kile,zaidi ya kutuambia nyie nyamazeni tutawaletea maendeleo wakati
yeye anaishi Dar es Salaam kwenye jumba zuri,tunafahamu ya kuwa anazo pesa nyingi sana ambazo hata kama akitokea mtu mwingine wa kugombea atamshinda tu.

Mh. Rais tumechoka kutawaliwa na watu wenye pesa kama hawa, hawatujali kabisa hasa pale wanapopata ubunge ,udiwani.Kazi yao ni kupeana posho lakini sisi wananchi tunaendelea kuteseka na hali ngumu ya maisha na kukoswa huduma kwa jamii.Tunashindwa kufahamu sisi tarafa ya Nyanja tunapewa kiasi gani cha pesa kutoka central government wakati wa budget,mbali . Mbali na hilo Mbunge ameshindwa kutuelezea matumizi ya pesa hizo ,Mkuu wetu wa wilaya hatujawahi kumwona zaidi ya kwenda ofisini kwake pale musoma Mjini.

Mh Rais imefikia wakati tunataka serikali yetu iwe ya wazi kwa
wananchi ili kwamba tufahamu ni nini kinachofanyika kwetu,wabunge na watenda kazi wanakula 10% kila kukicha,chukulia walimu hawaingii
darasani lakini ikifika mwisho wa mwezi wanalipwa na kuna walimu wengi ambao ni hewa na wanaendelea kulipwa mishahara.

Mh Rais kuna kipindi tuliomba jimbo ili likatwe mara mbili ili kwamba
na sisi tuwe na mbunge wetu,lakini lilipofikishwa katika mkutano wa
halmashauri kuu ya taifa ya CCM ,mbunge wetu alitupilia mbali hoja
yetu.Sababu kubwa ni Tarafa ya Nyanja ina vyanzo vingi vya utajiri
hasa samaki na dagaa ,pia kuna madini mbali na hilo kuna wapiga kura
wengi .Kwa Mh Rais tunahitaji kwa lazima kwa kufuata taratibu za
serikali ili na sisi tuwe na jimbo letu linalojitegemea. Mh.Rais
tunahitaji jimbo ili likatwe mara mbili ikiwezekena iwe ni wilaya
inayojitegemea.Au kuna sifa zinazohitajika kuwa wilaya?

Mbunge wetu anapoenda kwenye vikao vya bunge hatusikii chochote zaidi ya kusema amejenga shule lakini ukitazama shule nyingi zimejengwa upande wa kwako ,hii inaonyesha ubaguzi ambao na sisi hatuutaki kabisa,na pia hatutaki tufikie kukatana mapanga kama ilivyokuwa Rorya.Tumemchoka Mkono

Mh Rais kuna hii Basket Fund je na sisi tunafaidika vipi na huu mfuko
hasa vijijini?Mbali na hilo hatuna huduma zingine kama bank,vituo vya
polisi je lini huduma hizi zitawekwa?.Hata pia viongozi wa juu wa
Serikali wakija wanafikia Butiama na Wilaya zingine au kusikia Rais ,
Wawaziri ,Mkuu wa Mkoa amekuja kututembelea sisi wananchi zaidi ya
kuishia Butiama,tatizo lipo wapi?Kwanini wajita wamesahaurika katika
nyadhifa za juu za serikali hasa kwenye uwaziri na sekta zingine
?Tangu wakati wa Mwl Nyerere mpaka leo hii bado tupo nyuma jetulikosea nini Serikali ya Jamhuri ya Muungano?.

Mh Mbunge (Mkono) amekuwa akija kwetu hasa kwa sabubu ya uchaguzi ambao umekaribia,na kutoa vijipesa vidogo kwa wananchi na kuhaidi kutuletea au kuto mabati kwenye mashule ,Na pia kukutana na baadhi ya viongozi wa Tarafa na kuwapa pesa kidogo ili waanze kampeni taratibu kwa wananchi .Sisi tunasema hapana hizi pesa chafu hatuzitaki kabisa na hazituletei maendeleo katika tarafa ya Nyanja. Tunafahamu anazo pesa nyingi sana na anaweza kufanya chochote ili aendeleaa .

Mh. Rais sisi wananchi na hasa kupitia wazee wetu ambao hawana uwezo wa kujieleza hasa kwa Kiswahili wameshindwa kuelewa uongozi wa huyu Mbunge tajiri Mkono,Kwani yeye ni Butiama tu na sehemu zake hasa upande wa kwao ndizo anazoendeleza na kutafuta wafadhili.

Sisi hatutaki Mbunge tajiri tena mfanya biashara kwa sababu hawa ndiyo chanzo cha kuwepo na vurugu ,rushwa na pia hawatusaidii .Tunadhani kutoka na kauli yako ulisema wabunge wafanya biashara ndiyo mwisho wao wa kugombea ubunge kwani wanaharibu sifa ya nchi yetu Tanzaia ,wanatumia pesa zao chafu kutuharibia nchi na amani na utulivu tulio nao.Tunaomba kama ikiwezekana tume ya kudhibiti rushwa itumwe huku kwetu kutadhimini hali ya uchaguzi wa mwakani 2010.pesa chafu zinameanza kutembezwa.Tunafahamu ya kuwa Mkono ni mjumbe wa NEC ila hasitumie ubavu wake ili kwamba kwenyekura za maoni apitishe. Wajita tumechoka kununuliwa kwa pesa Mh.Rais tunahitaji maendeleo yanayoonekana na pia serikali iwe wazi inapotoa fedha hasa kwenye tarafa yetu.

Kilio chetu tumekuwa nacho zaidi ya miaka 10 na hakuna ufumbuzi wa
matatizo yetu inawezekana unaletewa reporti yenye kupotosha , kwahiyo sisi wananchi kupitia wazee wetu tumeona leo tuchukue jukumu la kukuletea wewe mh rais ili jambo kabla ya mwaka kuisha kwa kupitia vyombo vya habari,

Tumemchoka Mbunge wetu kabisa japokwa anadai ya kuwa hakuna wa
kumwondoa mpaka hapo atakapoachia madaraka,pesa anadai anayo na viongozi hakuna wa kumtoa hata wewe Rais .Tukimpigia simu kutoa shida anatujibu vibaya kiongozi gani asiye tujali sisi tuliomweka
madarakani?.

Mh.Rais uchaguzi umekaribia sana tunafahamu sana utashinda tena
kupitia tiketi ya CCM na tutakupatia kura zote ila mbunge wetu hapana
tunaomba mtupatie jina ili kwamba sisi wananchi tumchague ., tumechoka kununuliwa kwa pesa chafu ambazo hatujui zimetoka wapi , sasa Mh Rais tumeamka na macho yameona mbali .Tunasema , RUSHWA HAINA MAHALI PAKE TENA, Sisi Tarafa ya Nyanja tunaomba wananchi wenzetu walio na matatizo kama yetu hasa wa Vijijini tusinunuliwe kwa rushwa ya baiskeli kwani inatulemaza kabisa.

Rais tunakuomba haya matatizo utupatie ufumbuzi wa kina hasa katika
Tarafa yetu ya Nyanja na pia tunakuomba kabla ya kuanza kampeni uje Tarafa ya Nyanja na kama siyo wewe basi waziri Mkuu.

Tunakutakia Heri ya Mwaka Mpya 2010

WANANCHI TARAFA YA NYANJA MAJITA MUSOMA VIJIJINI

8 thoughts on “Barua Kwa Raisi Kikwete Toka Kwa WANANCHI TARAFA YA NYANJA MAJITA MUSOMA VIJIJINI

  1. Edina Lugano

    Natoa pongezi kwa wananchi wa tarafa ya Nyanja Majita kwa kuwa na uthubutu huu wa kumuandikia barua Mh. Rais na kutoa dukuduku lenu.

    WanaBidii mengi yaliyoelezwa katika barua hii yanaonesha kuwa:
    1. Nyanja Majita ni tarafa iliyo NYUMA KIMAENDELEO (kama yalivyo maeneo mengi ya vijijini hapa Tz); huku huduma muhimu za kijamii kama afya. elimu, maji, nk zikiwa ovyo.
    2. Wananchi hawa (sijui wanapi walishiriki kutoa mawazo yao) WANADAI HAKI YAO YA KIMSINGI YA KUPATIWA TAARIFA ZA FEDHA KATIKA ENEO/ HALMASHAURI YAO.
    3. Kiini cha matatizo yao wameeleza ni MBUNGE WAO KUTOA MISAADA/ HUDUMA KWA UPENDELEO na KUTOWASILISHA MATATIZO YAO KUNAKOHUSIKA.

    Sitazungumzia namba 1 & 2 kwani linaeleweka wazi. Msingi wa maoni yangu ni hoja ya wanajamii hawa wa Nyanja kuwa MBUNGE WAO HAWASAIDII KATIK KULETA MAENDELEO na ANAWADHARAU.
    Ndugu zangu wa Nyanja hili si suala la KULIPELEKA KWA MH. RAISI kwa maana HANA JIBU na hata angekuwa na jibu HANA MAMLAKA YA KUAMUA LOLOTE JUU YA MBUNGE WENU. Uwezo huo mnao ninyi (NDIO MNAOMPA AJIRA KILA BAADA YA MIAKA 5). Mbunge wenu ni miongoni mwa wabunge waliokaa kwa muda mrefu katika majimbo yao na mara nyingi hupita bila kupingwa. Naamini na wanaNyanja pia mnapiga kura (na hata kampeni mnamfanyia). Mmeshika mpini wa kisu ambacho pia ni mali yenu; mnao uwezo wa kuamua nini hatima yenu badala ya kulalamika kwa mheshimiwa Rais. Mmesema tarafa hii ina kata 12 (ni eneo kubwa lenye idadi ya wapiga kura wa kutosha mnaoweza kuleta mabadiliko).

    Kulalamika “mbunge/diwani/ mwenyekiti wa mtaa hatufai” imekuwa ni tabia yetu watanzania lakini ajabu uchaguzi ukifika yule asiyefaa tunampigia debe na kumuimbia na kumpamba sana; KISA KATOA TAKRIMA!
    Mwenyekiti wa wilaya wa Chama tawala katika jimbo moja magharibi wa Tanzania aliwaambia wajumbe na wananchi wa eneo lake mwaka 2005, “Je, kiasi cha fedha ulichopewa kinaweza kulipa karo ya mwanao kwa miaka miatano? Kinaweza kulipa gharama za matibabu kwa miaka? Chakula ulichokula hitahitaji chakula tena kwa miaka mitano? Je, kinawakilisha heshima, utu na uwezo wako wa kufanya maamuzi sahihi? Kwa kujibu maswali haya fanyeni maamuzi sahihi”.
    Walitafakari wakaona mantiki ya kauli hii; wakafanya maamuzi “SAHIHI”.

    WanaNyanja Majita kipimo cha kuwa MMECHOKA NA HALI YA MAISHA MLIYONAYO huku UWEZO WA KUYABADILISHA UPO NA MNAUONA ni mwaka huu 2010. UFUNGUO kuingia MAISHA BORA mnao. UWEZO wa KUAMUA ni wawakilishi (madiwani na mbunge) wa aina gani mnaowataka mnao (ingawa sijui mliamua nini 2009 katika uchaguzi wa serikali za mitaa).

    Kumtwisha Mh. Raisi Kikwete mzigo “wa kumshitaki mbunge wenu kwake” ni kumuonea kwa kumuongezea mzigo usiomuhusu! Tayari Mheshimiwa kalemewa; MSAIDIENI KWA KUMPATIA VIONGOZI (Mbunge na Madiwani) MAKINI wenye UWEZO WA KUSIMAMIA MAENDELEO YENU!

    Lugano E.

  2. maurice oduor

    Edina,

    This is a good advice you have given the elders from Nyanja. In Kenya, people will take your money during the campaigns but then end up voting for the candidate they want. This is what Nyanja residents should do. I am willing to help them understand this. This will send a strong message to all Tanzanians that they can no longer be fooled by politicians.

    Courage,
    Maurice

  3. john mahaba

    jamii injayojielewa haisubiri kuletewa maendeleo na mtu au taasisi<

    poleni ndugu zangu wa NYANJA kwa kero zenu zinazowakabiri kama ni kweli mwandishi ni mkaazi sahihi wa eneo hilo au ni wale waletwa na X-MASS NA MWAKA MPYA?

    Niwapongeze kwa kujijingea shule za sekondari 15 hapo hapo niwalaumu kwa kupoteza uelekeo baada ya kujenga hizo shule, nasema mmepoteza uelekeo kwani baada ya ujenzi huo mliamua kukaa na kumsubiri mbunge wenu ili awafanyie kila kitu na ambacho kimekuwa chanzo cha malalamiko yenu,

    Kwa watanzania tayari tumeanza huu mwaka wa kwa mbwembwe za aina yake na hii ni baadhi ya mbinu hizo kwani kwa wale wanaoelewa vizuri kila mwaka wa uchaguzi huibuka mambo mbalimbali likiwemo hili na matokeo yake huwavuruga wananchi kiasi wakati wa uchaguzi wananchi hufanya maamuzi mabaya.

    Tarafa ina vyanzo vya kudumu vya mapato lakini wananchi wameshindwa kujiletea maendeleo eti tatizo mbunge haleti maendeleo kweli?

    Tarafa ya NYANJA imeanzishwa mwaka gani hadi leo hii ndio tuanze kumlaumu mbunge? je waliomtangulia walifanya nini?

    mbunge hana uwezo wa kuwalazimisha wapiga kura kumrudisha kwenye nafasi hiyo basi kama kweli tumeona mapungufu yake atakayeyaondoa si Rais bali ni nyinyi wapiga kura wa jimbo la Musoma vijijini,

    kwa maoni yangu mantiki ya barua hii inaweza kuwa nzuri lakini imekosewa pa kuipeleka
    binafsi nafikiri hii ilitakiwa ifanyiwe kazi na wananchi wa jimbo/Tarafa hii badala ya kuipeleka kwa Rais

    rudisheni juhudi mlizokuwa nazo wakati wa ujenzi wa shule za sekondari na mjiwekee mikakati ya kutekeleza shughuli za maendeleo, malalamiko yanavunja ari ya kazi.

  4. maurice oduor

    John, you sound like a CCM apologist. You have completely trivialized the honest complaints from the residents of Nyanja. You should have been giving them ideas on how to work with their MP or get rid of him if he is useless to them.

    Courage,
    Maurice

  5. jovias mwesiga

    Wajumbe naomba kueleweshwa, hivi kwa muundo wetu wa madaraka mbunge kama mbunge anaweza kupeleka vipi maendeleo jimboni kwake?

    Swali hili limekuwa likinisumbua sana na hata nilipojaribu kuangalia mijadala ya bungeni inavyoendeshwa sikuona mahala ambapo nitaweza kumbana mbunge wangu kuleta maendeleo jimboni.

    Mfano ujenzi wa barabara mbunge akiwa jimboni anasema nitafanya hiki, diwani then mawaziri lakini kila kitu naona kinakwenda vuru vuru.

    Hebu nieleweshwe mbunge anacontrol gani ya hela ya maendeleo ya halmshauri ya jimbo/wilaya husika?

    Kama kuna mtu anaufahamu naomba kueleweshwa hela za makusanyo ya halmashauri ya wilaya huwa zinatumika vipi kwenye upangaji wa maendeleo husika?

    Naamini kama kila wilaya inayonjia nzuri ya ukusanyaji wa mapato, then wananchi wangekuwa wanapata maendeleo kupitia halmashauri zao.

    Ni hayo tu jamani

  6. JOSEPH MAX

    Ni kweli kabisa yaliyosemwa na wananchi wa Nyanja.Hata mimi nimekuwa najiuliza kuhusu mchango wa mbunge huyo katika eneo la Tarafa ya NYanja.Hayo ndiyo matatizo ya viongozi wanaoingia madarakani kwa Rushwa.Kwa kweli Mheshimiwa Mkono anapaswa kuwajibu wananchi hawa.Lakini pia wananchi wa Tarafa ya hiyo wanapaswa kutambua haki zao za kupiga kura.MKONO amekuwa akiwanunua kila wakati wa uchaguzi kwa hayo mabati na mifuko ya saruji.Kweli Tarafa hiyo ni tajiri kwa raslimali lakini ndiyo masikini kati ya tarafa zote.Kama tayari wametambua ugonjwa walio nao basi hakuna watakachoshindwa kwani wao ndio wapiga kura wengi katika jimbo hilo.Mwaka huu wasifanye makosa tena.Aidha mheshimiwa RAIS azingatie malalamiko ya wananchi na ayafanyie kazi.UMEFIKA WAKATI sasa Tarafa ya nyanja Ipatiwe UMEME. Kama ukerewe wameweza,je kwa nini wao wshindwe? Tatizo linalowakabili wananyanja ni ubinafsi.Kuna watoto wao wengi wamekatalia Dar es Salaam na kufanyia biashara zao huko, hawataki kurudi nyumbani. Mkono aliamua kurudi nyumbani, hivyo wasimtegemee sana.MTU KWAO BWANA.

  7. mswahili

    ni ajabu kuona hadi leo kuna kitu kinaitwa blog ya wajaluo, hivi ukabila utawapeleka watu ndugu zangu? na mbona mnataka kuleta ukabilahadi Tz, huku tz hatuhitaji ukabila wenu…cha ajabu, wajaluo ni kabila dogo sana tz na hawana nguvu yoyote hata kama mtawafanya kuwa extremists. ni wachache mno…hivi mnaonaje kama ungeifanya hii thread kuwa blog ta WAKENYA na sio wajaluo?ni ajabu sana ndugu zangu majirani hebu badilikeni…

    cha ajabu kwenye blog hii nimeona kuna chuki nyingi sana dhidi ya tz, watz wengi hawaijui hii tovuti na chuki zenu zote haziwafikii hivyo mnapoteza muda wenu tu.

  8. MPWAGA ALEXANDER YOHANA

    Nafasi ya wasomi katika uchaguzi mkuu wa Tanzania.
    Kwa mara ya kwanza ninajitokeza katika medani za siasa za Tanzania. Mimi ni mwanafunzi wa mwaka wa pili katika shahada ya sayansi ya uchumi kilimo katika chuo kikuu cha Sokoine cha kilimo (SUA). Nimejitokeza katika safu hii kueleza masikitiko na mtazamo wangu juu ya demokrasia ya watanzania kuchagua viongozi wao.
    Nimejiuliza kwa muda mrefu kama tunaandaa kizazi chenye mwelekeo kwa maendeleo ya taifa letu. Maana ninaamini madiliko yanaanzia kwenye uchaguzi endapo tutachagua na kuwapata viongozi bora na sio bora viongozi. Kulingana na mwelekeo na utaratibu unaofanyika unaonesha kuwa tunaandaliwa viongozi bila kujali tutaathirikaje katika kizazi kijacho kitakachokosa mwelekeo.
    Katika makala hii ningependa kujua nafasi ya wanafunzi wa chuo kikuu katika kuchagua viongozi wetu watakao tuongoza kwa miaka mitano ijayo. Katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005, wanafunzi wa vyuo vikuu walijiandikisha katika daftari la kudumu la wapiga kura wakiwa katika majimbo yao ya uchaguzi lakini uchaguzi ulifanyika wakati wanafunzi wengi wakiwa vyuoni hivyo kukosa haki yao ya msingi ya kuchagua viongozi wanafikiri wataleta maendeleo kwenye nchi yetu Tanzania. Mwaka huu 2010 wanafunzi wa vyuo vikuu tumeandikishwa katika daftari la kudumu la wapiga kura tukiwa vyuoni tukitegemea kupiga kura tukiwa chuoni lakini serikali ilitoa tamko kuwa vyuo hususani vya serikali vitafunguliwa baada ya uchaguzi mkuu hivyo kukosa haki yetu ya kuchagua viongozi kwa maendeleo ya taifa letu. Hata hivyo mwezi wa saba kulitolewa muda wa marekebisho, tulishindwa kurudi kwenye majimbo yetu ya uchaguzi kwani tulikuwa kwenye mitahani na mara baada ya mitihani tulitakiwa kuripoti kwenye vituo vyetu vya mazoezi ya kazi kwa vitendo (field practical) na kushindwa kufika kwenye wilaya zetu kwa marekebisho hayo.
    Je, hakuna uwezekano wa kuwepo utaratibu mzuri kwa ajili ya wanavyuo kupiga kura? Na kama utaratibu huu utaendelea tutapataje viongozi wazuri kwa kuwa wasomi wenye uwezo wa kusikiliza na kuchanganua hoja za wagombea? Je, tume ya uchaguzi haijaliona tatizo hili au mpaka watu walalamike ndipo waje na utatuzi? Je, kwa hali hii demokrasia inazingatiwa? Je, serikali inafanya nini kutoruhusu hali hii iendelee? Kama watanzania wenye mapenzi mema na nchi yetu tungependa kupata haki zote za msingi ili kuleta maendeleo kwa kizazi kijacho.
    Mpwaga Alexander Yohana
    mpwaga@yahoo.com
    0762 856769/ 0714 664922

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *