Tanzania: Miaka 49 ya Uhuru Tanganyika.

Miaka 11 bila Sanduku la Agano.

Na Douglas Majwala.

Mnamo 9-12-2010 taifa lilifikia kilele cha maadhimisho ya miaka 49 ya uhuru ambao wengi wanautafsiri kuwa ni wa bendera tu kwa maana licha ya nchi hii kuonekana paradiso lakini bado raia wake zaidi ya 75% hawawezi kumudu milo 2 kwa siku hata kwa mboga ya kauzu wasiojaza hata kiganja na kupelekea kuupa umaarufu ule usemi kuwa “usicheze mbali unga robo” huku wengine wakihoji kwa ukali ni lini ndani ya kipindi cha miaka 49 watanzania waliwahi kuambiwa “haya sasa legezeni mkanda mle mnywe msaze maana kesho itajiju”.

Ni aibu ya millennia kwa taifa lililojaliwa wasomi na viongozi waelewa mpaka wengine tunadiriki kuwafungulia milango watokomee ugahibuni kwa njia ya brain drain ingawa wao wanasema hailipi kutumika Tanzania kama inavyolipa ukitumika nje ya mipaka yake, kupoteza dira ya maisha. Taifa limeshindwa kuelewa kiundani kabisa sababu za kitaalamu zinazopelekea lishindwe kutumia rasilimali ya wasomi wengi iliyonao kujiletea maendeleo ukilinganisha na wasomi waliokuwa hawazidi 7 tu hivi wakati nchi inapandisha bendera yake kuashiria kupatikana uhuru pale uwanja wa taifa siku ile ya 09-12-1961 ambao licha ya idadi yao ndogo iliyovunja rekodi Afrika, walitumika na kuweza kuliweka taifa katika mustakabali unaoeleweka ambao ndiyo uliweka misingi ya kuliwezesha kupumua pasina mpira wa oxygen mpaka pale alipoondoka Musa [Baba wa taifa] na sanduku la agano. Je, ingekuwa siku ile ya uhuru ndiyo taifa lingekuwa na idadi ya wasomi iliyo nao leo hii nafikiri hata Marekani wasingetufikia ki-maendeleo.

Kwa hiyo hapa hoja ni mmoja tu kuwa ni jinsi gani kiongozi ana uwezo wa kujipanga na idadi ya rasilimali aliyonayo kujipatia maendeleo kama Mwl. alivyoweza kuipa nchi maendeleo [elimu bure, afya bure, ajira bure, miradi ya maendeleo nk bila kukusanya kodi] akiwa na wasomi 6 tu akiwemo yeye wa 7, akaweza hata kuwapanga vizuri wazungu waliokuwepo kuziba mianya ya wasomi wazalendo waliokosekana. Wazungu waliokuwepo katika utumishi wa umma walipangwa vilivyo kulitumikia taifa, ambapo leo hii tunao katika sura ya magabacholi ambao wanalihujumu tu taifa kutokana na kwamba hakuna Nyerere wa kuwapanga vizuri.

Pamoja na idadi kubwa ya wasomi, siasa safi, uongozi bora, watu na ardhi kubwa yenye rutuba bado taifa limeshindwa kusimamia siyo tu rasilimali asilia iliyonazo bali hata miradi mingi ya maendeleo iliyoanzishiwa na mzungu. Hali hii inafanya nguzo hizo nne za maendeleo zilizoasisiwa na Mwl Nyerere leo zitumike kinyume na maana yake [watu duni, siasa za maji taka, uongozi wa kifisadi na ardhi isiyomilikiwa na raia bali na wawekezaji wasioitumia kwa manufaa ya taifa] ndiyo maana taifa limefika kikomo cha maisha kama tunavyoshuhudia hivi leo.

Warasimu wa kisiasa wameliingiza taifa katika mchezo haramu wa karata tatu pale walipopambana mithili ya simba mwenye njaa kali aliyejeruhiwa na aliyekosa mawindo sasa akijitahidi kulipiza kisasi, pale ambapo waliandaa mazingira ya mauti ya ujamaa wa Mwl kwa njia ya kubadili mfumo toka mmoja kwenda mwingine kwa kigezo cha mabadiliko ya dunia nzima ambapo ujamaa wa Mwl tunaoulilia leo ulianza kushuhudia ujenzi wa kaburi lake na uchongeshaji wa jeneza lake siku baada ya siku huku ubeberu wa mitaji ya kimataifa ukikaa mkao wa kula na kukaa eda katika tanga la ujamaa wa Mwl kusubiri mirathi ya mashirika ya umma yaliyofilisiwa kutangazwa na msimamizi wa mirathi hizo yaani tume za kurekebisha mashirika ya umma. Nasema ujamaa wa Mwl kwa sababu ujamaa wa Fidel Casto na ule wa Mao Tsetung [haijalishi ameishakufa] bado vimebaki kuwa mfupa ulioshinda ubeberu.

Hapa ndipo wenye mamlaka wakaanza kumili hisa katika makampuni wakisajili hisa hizo kwa jina la Paulo kumbe kwa ukweli wanaitwa Sauli tena wanafanana na Sauli mpaka na roho zao huku kanisa nalo likishindwa kukemea kwa vitendo mweleko ambao taifa limechukuwa. Kanisa limekuwa kama limebariki hali hii kwa sababu kanisa halisi ambalo limebeba kusudi la MUNGU ndani yake ni kama kanisa la nyakati za biblia ambapo lilikuwa kimbilio la wenye mahitaji kama akina Batimayo ambao walijipanga kila jumapili langoni mwa hekalu [kanisa] kusubiri neema na wakaja wakapokea mpaka na neema ya uponyaji pia, leo kanisa limekuwa ndiyo mkimbizi kwa watu hata mafisadi badala ya watu ndiyo waone kuwa kanisa ni kimbilio lao [hali imekuwa kinyume].

Tunapoadhimisha miaka 49 ya uhuru ndani ya njaa kali, uchi mkali, magonjwa sugu na milipuko mipya, siasa viza, ufisadi uliotamalaki, chuki, majigambo, uhasama, fitina, husuda, vita vya koo, vita vya wafugaji na wakulima, ukame, giza totoro ndani ya mito isiyokauka, maji kwa vibaba [mgawo] ndani ya mito iliyotapakaa kila mahali, mpasuko wa vyama vya siasa kutokana na siasa za mchafuko wa bahari, undugunaizesheni wa kupindukia nk, kanisa nalo linaadhimisha sambamba miaka 49 ya utumishi wake ndani ya uhuru huo wa taifa [japo kanisa lilianza kabla ya uhuru] ambalo kanisa likishirikiana na dini zingine zimezalisha makuhani wake toka ndani yao [miongoni mwa waumini wao] kwenda kuliongoza taifa.

Viongozi wamebatizwa kanisani na nyumba zingine za ibada za imani nyingine pia, wana vyeo makanisani na nyumba zingine za ibada mbadala na wamekulia ukristo na imani zingine pia kwa maongozi ya kanisa na dini zingine lakini wameshindwa kuubwaga mathalan kwa wakristo “U-Sauli na kutwaa U-Paulo”, kwa maneno mengine ni kuwa taifa linaanzia kanisani/misikitini. Makanisa na misikiti ndiyo hutengeza taifa na uongozi wake pia, lakini utashangaa makasisi wakipiga domo madhabahuni nyakati za sikukuu za kidini wakipamba vichwa vya vyombo vya habari kwa kuisema serikali kwa jazba wakati wanasahu kuwa wao ndiyo wamewaandaa toka makanisani/misikitini mumo humo!!??

Mbona mahala pengi tumeona makasisi wakilikomboa taifa e.g. Zimbabwe ambapo Askofu Pius Ncube alimtafsiria Mugabe maneno “Mene mene tekeli na peresi” na mwisho wa siku tukaona Zim ikibadilika kwa kuikubali serikali ya mseto, bado pia historia haitamsahau Mchg. Canaan Banana ambaye pamoja na ma-comrade wenzake waliiletea Zim uhuru, dunia pia haitamsahau Askofu Mkuu Desmond Tutu wa Afrika Kusini alivyoendesha mapambano ya kudai ukombozi kutoka ubaguzi wa rangi akitumia silaha ya biblia na kola ya uaskofu, pia Askofu Mkuu Okulu na Muge wa Eldoret waliofanyika mwiba mchungu kwa serikali babe ya Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Kenya Daniel Toroitich Arap Moi.

Inashindikana nini Tanzania? Ni uongo mkubwa kutenganisha siasa na kanisa/msikiti, hizi taasisi mbili [kanisa/msikiti na serikali] zinaushirika wa toka enzi na enzi, hata Israel bila kanisa hakuna serikali [wanajeshi wake huenda vitani kwa imani ya kiroho zaidi ya silaha kali walizonazo na ndiyo maana wana jeshi linaloogopewa duniani mithili ya sisimizi na siafu wanavyoogopwa na tembo], Upalestina huwezitenganisha dini na serikali, Uingereza malkia ndiyo mkuu wa ngazi ya juu kabisa wa kanisa la Anglikana na pia ndiye mkuu wa ufalme, Saudi Arabia, Indonesia, Irak, Pakistan nk hali ni hiyo hiyo.

Sanduku la agano alilokabidhiwa Mwl Nyerere wakati wa uhuru liko wapi? Alimpa nani wakati anaenda St.Thomas London ambako alirudi akiwa ndani ya galadi? Miaka 11 bila Mwl na bila sanduku la agano imebadili kabisa sura na mwelekeo wa taifa mpaka watanzania leo wakiona jambo linaenda mrama basi utawasikia wakisema “ kama Mwl angekuwepo hili lisingekuwa hivi badala yake lingekuwa vile”, na sasa watanzania wamekuna vichwa kwa muda mrefu na hatimaye wakapata mafunuo kuwa mustakabali wa taifa umeshindikana kutokana na kutoweka kwa sanduku la agano na sasa wameanza kulitafuta kwa jasho hata la damu maana pasina sanduku hilo lazima maadui kama njaa kali, uchi mkali, magonjwa sugu na milipuko mipya, siasa viza, ufisadi uliotamalaki, chuki, majigambo, uhasama, fitina, husuda, vita vya koo, vita vya wafugaji na wakulima, ukame, giza totoro ndani ya mito isiyokauka, maji kwa vibaba [mgawo] ndani ya mito iliyotapakaa kila mahali, mpasuko wa vyama vya siasa kutokana na siasa za mchafuko wa bahari, undugunization wa kupindukia, demokrasia tete, uchumi dororo, pato hafifu la taifa, gharama za maisha kupaa, viwango vya maisha kushuka mpaka chini ya mstari wa umasikini, mparaganyiko wa utumishi wa umma unaoleta migomo na mitafaruku ya kazi, mikataba ya uwekezaji wa mitaji ya kimataifa iliyoliweka taifa njia panda na kulivua nguo bungeni na kwenye foramu za wanaharakati nk wataishambulia nchi yao!! Tusubiri miujiza ya kubadili jina kama ilivyokuwa kwa Abraham kwenda Ibrahim na Sarai kwenda Sara ndipo maisha yao yakabarikiwa na kupata Zawadi ya Isaka au hata Sauli kwenda Paulo ndipo agano jipya kwenye biblia likajipatia nyaraka nyingi kupitia mkono wa wokovu wa Paulo?

Tanzania inaingia miaka 50 ya uhuru [golden-jubilee] 09-12-2011 bila kupishana sana umri na Korea Kusini, Taiwan, Hong Kong, Indonesia, Malaysia na Thailand lkn nchi hizo zimewezakuja na Marshal Plan isiyo ya miujiza mikubwa sana kama ya Eliya, bali ambayo hata Tanzania pia inaweza ikaifanya lakini wao wameweza kujenga Tiger Economies huku sisi tukishindwa hata kuota ndoto za Mini-Tiger Economy badala yake wenzetu wa United Arab Emirates wameweza kuota ndoto hizo za Mini-Tiger. Mataifa hayo ya mashariki ya mbali yote yalikuwa kambi moja ya South-South na Tanzania, lakini leo Tanzania imejikuta imebaki pale ikijishika tama huku hawa wenzake wamejipatia sifa za kutowafanya waitwe tena nchi za South-South, labda tuwaite nchi za dunia ya pili. Zab. 58.

majwalaoriko@yahoo.co.uk

0782299399.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *