Date: Mon, 29 Jun 2009 07:07:21 +0300
From: Constantino Kudoja
Subject: North Mara na Kilio cha Sumu
Taarifa hii nilipata kuiona Channel ten kwenye kipindi cha Pambanua Live.Kuna taarifa zinazosema kuwa walalamikaji walikuwa ni vibaka.Na taarifa kutoka kwa wamiliki wanasema ni taarifa za uzushi.Je ukweli ni upi juu ya jambo hili labda wanabidii waliopo karibu na migodi hii ya North Mara wanaweza kutuhabarisha.
Kilio hiki cha sumu mgodi wa North Mara kisipuuzwe
NA EDITOR
28th June 2009
http://www.ippmedia.com/media/picture/large/Tigithe.jpg
Mwanamke mkazi wa Tarime akifikiria kuchota maji yaliyochanganyika na sumu kutoka mgodi wa North Mara
Upo msemo kwamba ‘lisemwalo lipo na kama halipo, linakuja’. Ukiona jambo linazungumzwa sana, basi ujue ukweli wake uko mbioni kubainika.
Mwezi mmoja uliopita, gazeti hili toleo la Mei 24, mwaka huu, lilichapisha habari iliyokuwa na kichwa cha maneno ‘Mgodi wahatarisha maisha’…wamwaga maji yenye tindikali mtoni, mifugo yafa ovyo na mimea yanyauka.
Katika habari hiyo, wakazi waishio kandokando ya Mto Mara unaomwaga maji yake kwenye Ziwa Victoria wilayani Tarime, walitahadharishwa kutokula nyama ya mifugo ya aina yoyote itakayokufa eneo hilo.
Aidha wasitumie maji ya mto huo kutokana na tindikali ya asidi inayotoka kwenye mgodi wa North Mara kusambaa eneo hilo.
Tahadhari hii ilitolewa na Afisa Mifugo wa Kata ya Matongo tarafa ya Ingwe, Paskal Masele baada ya kupokea malalamiko ya kufa ng’ombe watano waliokunywa maji ya mto Tigithe ambao unatiririsha maji yenye tindikali kutoka mgodi huo na kuzimwaga katika mto Mara.
Afisa mifugo huyo alisema alipokea malalamiko ya mkazi mmoja toka kitongoji cha Konsara ulipo mgodi huo na kwamba baada ya kumtembelea mzee huyo alikuta wananchi wamekula nyama ya ng’ombe hao waliokufa, hali iliyomfanya apige marufuku wasile tena nyama ya mnyama mwingine atakayekufa.
Hiyo ilidhihirisha wazi kuwa lilikuwepo tatizo na kwamba madhara kwa watumiaji wa maji hayo yangeendelea kujitokeza.
Kwa wale waliokuwa wamekula nyama wa ng’ombe waliokufa, tayari walianza kubabuka ngozi ya mwili.
Pia sumu hiyo inayotokana na miamba inayochimbwa ardhini na kampuni ya Barick Gold ilionekana kuanza kuunguza miti na mimea yanakopita maji yanayotoka mgodini kuelekea mto Tigithe.
Wiki hii, gazeti moja la kila siku lilibeba habari iliyosema ‘Walioathiriwa na sumu North Mara watua Dar…Wataka serikali iufunge mgodi huo’.
Habari hiyo iliambatana na picha ya mmoja wa wakazi wa kijiji cha Matongo akionyesha jinsi ngozi yake ilivyoharibika baada ya kunawa maji yenye sumu yanayotiririshwa kwenye mto Tigithe kutoka mto huo wa North Mara.
Jambo hili lisifanyiwe mzaha, yafaa serikali ichukue hatua haraka kabla kizazi cha eneo hilo hakijatoweka.
Kilio cha tatizo hili kimetolewa wiki hii na Mbunge wa Tarime, Charles Mwera(Chadema), akimtaka Waziri Mkuu, Mizengo Pinda kutoa kauli ya serikali kuhusu hali mbaya ya wananchi wa jimbo lake hususani walio karibu na mgodi wa Nyamongo unaomilikiwa na Barick kuathirika kutokana na kemikali zinazotiririka katika maji wanayotumia wananchi.
Katika majibu yake, Waziri Mkuu alikiri kuona hali hiyo kupitia vyombo vya habari na kwamba hata yeye amesikitishwa na kuahidi kutuma ujumbe kulishughulikia haraka iwezekanavyo.
Tatizo hili limeripotiwa mwezi mmoja sasa na mbali na tahadhari waliyopewa wakazi wanaozunguka eneo hilo, hakuna kiongozi yeyote wa serikali, siyo waziri, mkuu wa wilaya wala mkuu wa mkoa aliyechukua hatua ya kufika na kujionea hali halisi.
Tunamini hivyo kutokana na ukweli kwamba, baadhi ya wakazi walioathirika wameshindwa kuvumilia hata kuamua kuja Jijini Dar es Salaam wakiamini kuwa pengine kilio chao kitasikika kwa karibu zaidi.
Jamani, kilio cha aina yoyote kile hakipaswi kupuuzwa. Yafaa kifuatiliwe mara moja ili tatizo nalo lithibitiwe kwa kupatiwa ufumbuzi wa haraka.
Hili la North Mara linahusu uhai wa watu. Athari za tindikali zinafahamika. Ni kitu kinachoweza kuonyesha madhara mara moja au athari za taratibu na inapofikia hata kudhihirika wazi, athari hizo ni vigumu kuzidhibiti.
Tulidhani kwamba mara tu baada ya kilio cha wakazi wale wa Kosara, serikali mara moja ingetuma ujumbe, ukiongozwa na waziri mwenye dhamana ambaye ndiye anayetia saini mikataba na wawekezaji, kwenda haraka kujua nini kilichotokea. Lakini hilo halikufanyika na sasa serikali inasema itatuma timu kubaini ukubwa wa tatizo.
Ni imani yetu kwamba tatizo hilo litafanyiwa uchunguzi wa kutosha ili kutatua hasa ikizingatiwa kwamba hata mwekezaji mwenyewe alishakiri kuwa tindikali ilikuwa ikiingia kwenye mto huo, ingawa alidai vifaa vya kuzuia vilikuwa vikiibiwa na watu wasiojulikana.
CHANZO: NIPASHE JUMAPILI
Constantino Mathew Kudoja
“I don’t believe in failure.
It is not failure if you enjoyed the process”
–~–~———~–~–
Huu ni unyama inaonyesha tunavyojali mali kuliko maisha ya raia