Nimejaribu kujiuliza kuwa hawa ndugu zetu ambao wamebatizwa jina la “Makamanda” wa vita ya ufisadi walioko CCM wanachopigania hasa ni nini? Ujumbe wao unaotufanya tusimame nyuma yao na kuwaunga mkono hasa ni kitu gani? Kama kuna mtu ambaye bado ni dhaifu na hajaamua kuchagua upande hawa wapiganaji watamshawishi vipi ili awaunge mkono; wanamuahidi nini?
Ninajiuliza maswali hayo na mengine mengi kwa sababu ukiondoa madai makubwa mawili bado najaribu kutafuta ujumbe wa wapiganaji wetu ili niweze kuelewa kama wana nafasi ya kushinda au watakuwa na athari ya kuvutia mikutano na kuuza magazeti na majina yao kutangaa lakini itakapofika muda wa kura wakajikuta wanatupwa nje ya ulingo.
Zafanana
Kitu kimoja hata hivyo naweza kukisema kwa uhakika zaidi ni kuwa kuna mfanano wa ajabu kati ya wanasiasa watetezi wa mafisadi (makuwadi wa ufisadi) na wale wanasiasa wanaowapinga mafisadi (wapinagaji). Kufanana huku ni muhimu kukuelewa kwani kimsingi kabisa kunafanya wapiganaji wawe na kazi kubwa zaidi ya kuushawishi umma kuhusu lengo na madhumuni yao hasa ni nini.
Wanafanana kwani makundi yote mawili yako kwenye chama kimoja; CCM imekuwa kama tenga lililobeba ndani yake matunda mabivu na matunda ambayo hayajaiva na pamoja na hao matunda wadudu wa kila aina wanaofuata uchafu. Makundi yote mawili yako kwenye tenga moja na hivyo moja linaweza kubeza jingine kuwa halijaiva sana au bado ni bichi au limeoza na lile jingine likalalamika kuwa linaonewa na kuwa kinachofanyika ni “chuki binafsi”. Lakini ukweli unabakia hadharani kuwa wote wawili wako kwenye tenga moja.
Wanafanana kwa sababu wote wanagombania nafasi ndani ya chama hicho hicho kimoja. Tumeshuhudia Dodoma wiki chache zilizopita jinsi gani makundi haya mawili yako kwenye muelekeo wa kugongana kusikoepukika. Lakini pamoja na mgongano huo tunaona kuwa makundi yote mawili yanagombania zaidi nafasi zao ndani ya chama. Hadi hivi sasa kundi la watetezi wa watuhumiwa ufisadi linaonekana kuongoza na kupata mashabiki wengi zaidi.
Ni nani kati yao atakayeweza kuwa na nafasi ya kutengeneza wagombea wa nafasi mbalimbali za uongozi hususan kwenye Ubunge ifikapo 2010? Itakuwaje kama kundi la makuwadi litapata kuunga mkono zaidi ndani ya chama na kundi la wapiganaji likajikuta linaungwa mkono zaidi nje ya chama? Jibu ni jepesi; makuwadi watakuwa na wagombea wengi zaidi chamani na hivyo kutuamulia viongozi wetu wajao ni kina nani.
Hata hivyo kufanana ninakozungumzia mimi siyo kufanana kwa aina hiyo. Ni kufanana kwa kile wanachogombania mwakani ni nini hasa. Makundi yote mawili yanagombania kuchaguliwa tena.
Baada ya matukio ya kihistoria ya Februari 2008 yaliyosababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu kwa kuhusishwa na kashfa ya Richmond mpasuko mkubwa umetokea ndani ya CCM. Mpasuko ambao hauwezi kuisha kwa vikao, mazungumzo, makubaliano au muafaka wa aina fulani. Mpasuko huu ni mkubwa sana kwani makundi mawili yanayoshindana hayawezi kurudi nyuma hata kidogo kwani kufanya hivyo itakuwa ni sawa na kujitia kitanzi wao wenyewe.
Kundi la watetezi wa Lowassa haliwezi kurudi nyuma kwani hawa wanaamini kabisa kuwa kitendo cha Lowassa kubanwa na kamati teule ya Bunge kilikuwa kimekusudiwa, kupangwa na kufanikishwa na watu mbalimbali miongoni mwao ni Spika wa Bunge la Muungano Bw. Samweli Sitta na aliyekuwa Mwenyekiti wa Kamati hiyo teule Dr. Harrison Mwakyembe pamoja na wajumbe wengine wa kamati hiyo.
Hivyo kundi hili la Lowassa, mashabiki wake, wanufaika wa utawala wake, mashabiki na marafiki wake wa karibu waliapa toka wakati ule kulipa kisasi na kuhakikisha kuwaangusha wahusika wote na hatimaye kusababisha mchakato mpya utakaomsafisha Lowassa na wenzake na kitendo kile wanachoamini kuwa ni cha “uonevu mkubwa”. Kama nilivyodokeza siku chache baada ya matukio yale kundi hili halitokoma mpaka Lowassa atakaposimama tena akiwa safi na akiwa kiongozi. Chini ya hapo hakuna mapatano.
Kundi la kina Mwakyembe linaamini kabisa kuwa lilifanya kazi yake kwa uadilifu na weledi na halikumuonea mtu yeyote na zaidi kuwa wangeweza kufanya makubwa zaidi kama wangetaka. Hawa wamejipanga wakati wowote kumwaga “mchele kwenye kuku wengi” endapo itabidi iwe hivyo hasa pale hatima yao ya kisiasa itakapokuwa mashakani. Kundi hili linaamini kabisa kuwa Ofisi ya Waziri Mkuu ilihusika moja kwa moja na suala la Richmond na kwa hilo hawako tayari kumuomba msamaha mtu yeyote.
Hawa nao mashabiki wao, wapambe wao na wale wanaowaunga mkono hawako tayari kurudi nyuma wala kusalimu amri. Sasa hawa wamepania kabisa kutetea viti vyao vya Ubunge na nafasi zao katika chama.
Hivyo basi tunaweza kuona kuwa pande hizi mbili haziwezi kupatana kwa kadiri ya kwamba kila moja inaamini kuwa iko sahihi katika mtazamo wake wa matukio ya Februari 2008. Hawawezi kukaa meza moja; hawawezi kujadili sera pamoja na kwa hakika kwa upande wao hakuna mapatano yoyote na wale wa utetezi wa kundi la ufisadi isipokuwa ushindi tu.
Ushindi hauji chee
Hapo kwenye ushindi ndio tatizo. Kama nilivyoanisha katika makala zangu kadhaa zilizopita ni kuwa vitani ushindi hauji mezani bila kumlazimisha adui kusalimu amri. Ushindi katika vita unakuja kwa kumzidi adui uwezo na kumuweka kama kwenye kabali hivi na kumlazimisha anyanyue mikono kuomba radhi na kuingia katika meza ya makubaliano ya kusitisha vita kwa kusalimu amri.
Ili upande mmoja ushinde ni lazima uwe na ujumbe, mbinu, na zana na utaalamu wa kutosha kumshinda adui. Nasikitika kusema kuwa upande wa watetezi wa Lowassa na wale wanaowatetea mafisadi (kama wanaomtetea Mkapa) umejipanga vizuri zaidi, ujumbe wake unagusa wanufaika wengi wa ufisadi na kwa hakika wana uwezo na zana za kuwamaliza wapinzani wao.
Ndio maana hapa nimeuliza hawa wapiganaji wetu wao wanaujumbe gani zaidi ya zile mbili tulizozizoea na ambazo ukweli wake unakubalika katika akili za Watanzania wengi? Ni zipi unauliza..?
Kwanza kuna ujumbe kuwa mafisadi wanaeneza fedha na mikakati ya kuwang’oa katika viti vyao vya Ubunge. Hili tumelisikia kwa muda na lina mantiki ndani yake. Kwamba, wale walioathirika wanataka kuwaangusha wale waliowaathiri ni sehemu ya siasa. Ninachokiona ni kuwa watetezi wa ufisadi wanatumia sayansi na sanaa ya siasa kuwaangusha wabaya wao. Katika hili mbinu na njia mbalimbali zitatumika hata zile ambazo ni kinyume cha sheria.
Sasa wapiganaji wetu wamekuwa wakilia na kulalamika juu ya hili. Lakini wataendelea kulia lia huku hadi uchaguzi mkuu utakapofika ili kiwe nini? Sawa mafisadi wanataka kuwaangusha kwenye majimbo ya uchaguzi wao walitarajia nini? Hivi walifikiri baada ya matukio ya Februari wangetumiwa zawadi ya maua na keki kutoka kwa walioangushwa kwa fedheha na aibu?
Wanachofanya makuwadi wa mafisadi si kingine bali kutumia siasa kulipa kisasi na Dodoma ilikuwa ni mwanzo tu. Watapiga tena.
Ujumbe wao wa pili ni kuwa kuna mafisadi na mafisadi ni lazima washindwe. Sasa ukweli wa huu tunaujua kuanzia enzi za kipindi cha “Mikingamo” na matangazo ya “Liangalieni limbukeni hili”. Mafisadi wamekuwepi nchini kwa muda mrefu na wamekuwepo ndani ya CCM kwa muda mrefu (na siyo wanne tu kama mmoja alivyotaka tuamini).
Sasa kutuambia kuwa mafisadi wanasambaza fedha na vipeperushi n.k kwenye majimbo katika mbinu ya kuwaangusha wapiganaji kunaweza kutufanya tuwaonee huruma lakini hiyo ni sehemu ya siasa. Kama watetezi waliweza kujipanga vizuri hadi kuweza kuleta hoja nzito dhidi ya Spika kwenye mkutano wa Halmashauri Kuu na kwa kutumia njia za kisiasa basi hatuna budi kukubali kuwa hii ni sehemu ya siasa na makuwadi wa ufisadi wako tayari kutumia mchakato wa kisiasa kutimiza malengo yao.
Pia kutuambia ukweli kuwa ufisadi na mafisadi wapo na wana nguvu na wako tayari kufanya lolote ni ukweli ambao wengi wetu tunaufahamu.
Wananchi wanahitaji na wanastahili zaidi ya jumbe hizo mbilli. Watanzania wanataka kujua hawa wapiganaji zaidi ya kupigana ili kuokoa meli zao kabla ya uchaguzi ni kitu gani kingine ambacho ni kikubwa na wanakipigania ambacho kitawafanya wananchi wawaunge mkono na kuwarudisha Bungeni?
Je, wao wapiganaji wanatumia vipi mchakato wa kisiasa kuwazidi kete makuwadi wa ufisadi? Je wanafanya kila kinachowezekana kuhakikisha kuwa makuwadi wa ufisadi na wenyewe hawarudi Bungeni na kushika nafasi mbalimbali?
Ninaamini katika mvutano huu ni ushindi wa upande mmoja tu utakaosababisha mjadala kuisha ndani ya CCM. Hadi hivi sasa wanaoelekea kushinda ni watetezi wa ufisadi na dakika ni hizi za majeruhi. Je, wale wapiganaji wetu zaidi ya kuhutumia mikutano ya kutupa jumbe zao mbili wana kitu gani zaidi wanachogombania ndani ya CCM na kwenye Taifa ambacho kitatufanya tuamini kuwa kitu hicho ni cha thamani zaidi kuliko fedha na ahadi za makuwadi wa ufisadi?
Ni kitu gani wapiganaji wetu wanagombania hasa ukiondoa wao kuchaguliwa tena kwenye Bunge la 2010?
—
Yona Fares Maro
I.T. Specialist and Digital Security Consultant
– – –
From: Yona Fares Maro
Date: 2009/9/8
Subject: WAPIGANAJI CCM WANAPIGANIA NINI?