LOWASSA ALICHELEWA KUJIUZURU

From: Yona Fares Maro
Date: 2009/11/4

LOWASSA HAKUONEWA; ALICHELEWA KUJIUZULU!

To: hollymaro

LOWASSA HAKUONEWA; ALICHELEWA KUJIUZULU!

Kuna baadhi ya watu ambao wanaamini mioyoni mwao kuwa aliyekuwa Waziri Mkuu na Mbunge wa Monduli Mhe. Edward Lowassa alionewa na Kamati Teule ya Bunge na kuwa alilazimishwa kujiuzulu kutokana na kutotendewa haki na Kamati hiyo iliyoongozwa na Dr. Harrison Mwakyembe, Mbunge wa Kyela. Watu wenye imani hiyo wanaamini kabisa kuwa Lowassa hakutendewa haki na hivyo wanafanya kila jitihada ya kuhakikisha kuwa Lowassa anasafishwa na hatimaye kujengwa tena ili kuweka rekodi iwe sahihi.

Katika makala hii ambayo nimeitengeneza kwa mtindo wa maswali na majibu nina kusudio la kuonesha kuwa Bw. Lowassa hakuonewa na mtu yeyote, alitakiwa kujiuzulu hata kabla ya Kamati Teule kuundwa na kuwa mjadala way eye kuonewa na chombo chochote ni mjadala unaotokana na mtazamo finyu, wenye ushahidi dhaifu, na kwa kipimo chochote unajaribu kutengeneza kitu ambacho hakipo. Ni makusudio yangu kuonesha kuwa Bw. Lowassa alistahili kujiuzulu mapema zaidi na hata pale alipochelewa alitakiwa kukubali adhabu aliyojipa yeye mwenyewe kutokana na kutokuwajibika kwake, uzembe wa ofisi yake, na kutokuonesha usimamizi unaomstahili Waziri Mkuu katika jambo nyeti kama la nishati.

Lengo kubwa ni hatimaye kulazimisha kwa nguvu za hoja kufunga mjadala huu baada ya kuzipima hoja zote kama zilivyo. Fuatana nami ukiwa na fikra huru ili uweze kuona kuwa nafasi aliyonayo sasa hivi Bw. Lowassa ndiyo nafasi ya juu kabisa ambayo anastahili kuishika katika Jamhuri yetu, ceteris paribus.

Swali:

Hivi karibuni makala ya gazeti la Nipashe imeonesha jinsi Lowassa alivyoshiriki katika mchakato wa kuipatia kampuni ya Richmond tenda, unaichukuliaje makala hiyo?

M.M. Kwanza niseme kwamba makala ile imeandikiwa kishabiki sana kiasi kwamba hata ukweli uliopo ndani yake unachafuliwa na ushabiki huo. Unapoandika habari za uchunguzi au kuibua kashfa au kufafanua jambo ni muhimu kuweka pembeni hisia zako juu ya jambo hilo au kutumia maneno ambayo katika ulimwengu wa hoja tunaita ni ‘kumshambulia mtu’ – ad hominem.

Licha ya ushahidi uliodaiwa kuoneshwa kwenye makala hiyo juu ya ushiriki wa Lowassa kwenye mchakato wa Richmond tunaweza kuona matumizi ya maneno ambayo yalikusudia au yamekusudia kuwafanya duni baaedhi ya washiriki. Kwa hiyo, Hivyo, makala ile ingeweza kuandikwa kitaalamu zaidi badala ya jinsi ilivyoandikwa kwa mtindo wa mipasho, vijembe, kejeli na dharau hasa kwenye jambo nyeti na zito kama hili.

Swali:

Makala imeonesha jinsi Lowassa alivyoshiriki katika mchakato wa kuipa Richmond tenda, kitu ambacho kuna watu wanadai kuwa hakuwa anashiriki huoni kuwa kuweka hilo wazi kulikofanywa na gazeti hilo kumefuta hoja hiyo?

Jibu:

Kwanza hoja siyo kushirki au kutoshiriki kwa Waziri Mkuu. Ukisoma vizuri makala hiyo utaona kuwa imemsaidia zaidi Lowassa kuliko kuonesha kuwa alichofanya si sahihi. Makala hiyo inaonesha sifa kadhaa ambazo kwa haraka haraka zinaonekana kumpamba Lowassa zaidi; ni mfuatiliaji, haogopi kuchukua maamuzi magumu, yuko tayari kufuatilia taarifa hata za mitaani, n.k Ndio maana mwitikio wangu wa kwanza kwenye makala hiyo ulikuwa ni kuwa gazeti la Nipashe limemsafisha Lowassa na kumfanya kuwa kweli ameonewa!

Swali:

Ina maana hiyo makala inamjenga Lowassa zaidi kuliko kumbomoa kama ilivyotarajiwa?

Jibu:

Bila ya shaka. Makala haioneshi ni makosa gani ya kisheria ambayo Lowassa aliyafanya kwa kuingilia mchakato wa tenda; haioneshi ni makosa gani aliyafanya kwa kutaka Richmond ipendelewe kupata hiyo tenda, na wala haioneshi ni tatizo gani linatokea pale Waziri Mkuu anapoamua kuunda chombo nje ya vile vilivyopo kisheria kufuatilia tenda. Hivyo, kwa mtu wa kawaida, utaona kuwa Lowassa anaonekana kama mtu aliyedhamiria kwa namna “yoyote” ile kuhakikisha kuwa suala la tatizo la umeme linakomeshwa mara moja. Kwa hiyo hiyo makala ilikuwa na udhaifu mkubwa sana na sijui ni vipi iliweza kutumiwa jinsi ilivyo!

Swali:

Sielewi; ina maana unaamini basi kuwa Lowassa hakustahili kujiuzulu kwani alikuwa anafanya alichotakiwa kufanya kama ushahidi unavyoonesha katika makala hiyo siyo?

Jibu: La hasha; ninaamini kuwa Lowassa alistahili kujiuzulu mapema zaidi si kwa kile tu ambacho kinaonekana katika makala hiyo au madai ambayo tumekuwa tukiyasikia bali kwa kitu kikubwa zaidi ambacho hakijaandikwa kwa kina kikaeleweka. Lowassa alistahili kujiuzulu kwanza kwa sababu alikiuka sheria, alijipa madaraka asiyokuwa nayo, na alishindwa kutumia nafasi aliyopewa kujitetea kujenga hoja kwanini ripoti ya Mwakyembe haikumtendea haki.

Swali: tafadhali fafanua kuhusu “kukiuka sheria”

Jibu: Wakati tatizo la nishati linatokea mwaka 2006 kama ilivyo kawaida serikali ikaanza kutafuta jinsi ya kulitatua. Ni lazima tutambue kwanza kabisa kuwa tatizo la nishati Tanzania siyo geni na hakuna mtu mwenye akili timamu ambaye anaweza kudai kuwa hatukujua kuwa tutakuwa na tatizo hilo kama vile lilivyotokea tena mwaka huu na kama itakavyotokea mwakani!

Zaidi ya yote ni muhimu kutambua kuwa tatizo la nishati la Tanzania halitokani na upungufu wa maji kwenye mabwawa yetu! Sababu hii imekuwa ikitajwa mara nyingi na wananchi wa kawaida wamekuwa wakikubali. Ni kisingizio dhaifu cha tatizo hasa la nishati nchini. Tatizo letu ni uongozi usio na maono, dhaifu kuamua, legelege katika kutenda na usiothubutu kujaribu mambo makubwa na kubakia kujaribu vitu vidogo kwa sababu vikubwa vinatisha! Tanzania haina sababu hata moja ya kuwa na tatizo la nishati ya umeme.

Tukielewa hilo tutaona kuwa mwitikio wa Waziri Mkuu wakati wa upungufu wa nishati hiyo mwaka 2006 ulikuwa ni wa jazba, hamaki, na uliojaribu kutengeneza kimbunga ndani ya kikombe cha chai au maporomoko ya maji kwenye kijiko.

Idara zote na taasisi zote za serikali zinaongozwa na Sheria ya Manunuzi ya Umma ya 2004. Sheria hii imeweka utaratibu wa jinsi gani wizara, idara, wakala au taasisi fulani ya serikali inaweza kununua vitu mbalimbali au kuuza vitu mbalimbali. Ni sheria inayohusu vyombo vya umma na hata vya binafsi ambavyo vinahusisha fedha za umma. Hivyo ni sheria hii ndiyo ilitakiwa kufuatwa wakati wa tatizo la nishati la mwaka 2006.

Swali: Sasa unasema kuwa hiyo sheria haikufuatwa?

Jibu: Jibu la moja kwa moja ni ‘ndiyo’. Sheria hii haikufuatwa ilivyotakiwa na matokeo yake ni kupatikana kwa kampuni ya Richmond kama mletaji wa majenereta ya kufua umeme. Ni kutokana na kutokufuatwa kwa sheria hii ndiko kulisababisha kampuni ya Richmond kupewa tenda, kushindwa kupatikana kwa majenereta katika muda uliotakiwa na hatimaye kusababisha kujiuzulu kwa Waziri Mkuu. Kama sheria hii ingefuatwa Lowassa asingekuwa katika nafasi iliyomkuta Februari mwaka jana. Hii ndiyo maana ya sheria ni msumeno.

Swali: Una mfano wowote wa jinsi gani sheria hii haikufuatwa?

Jibu: Ndiyo. Sheria ya Manunuzi ya Umma inasema wazi kuwa hakuna chombo chochote cha serikali kitakachotangaza, kutoa au kutia sahihi mkataba wa kununua kitu chochote bila ya kuhusisha Bodi ya Tenda ya taasisi hiyo na Mamlaka ya Manunuzi ya Umma. Ibara ya 31 ya sheria hiyo iko wazi kabisa. Kipengele (a) cha sheria hiyo kinasema wazi kuwa kinakataza jambo hilo na kipengele (b) kinasema wazi kuwa hakuna tenda yoyote itakayotolewa kwa mtu au taasisi yoyote isipokuwa kama imeidhinishwa na bodi ya tenda husika.

Swali: Nimekupata. Kwa hiyo kwenye suala la Richmond nani alitakiwa asimamie utoaji wa tenda?

Jibu: Katika suala hili chombo kilichotakiwa kusimamia mchakato wa upatikani wa tenda ni Bodi ya Tenda ya Shirika la Umeme la Tanzania (TANESCO). Ni chombo hicho peke yake kuanzia mwanzo hadi mwisho kilichotakiwa kutangaza, kuchuja, kupima, na hatimaye kuingia mkataba na kampuni iliyotimiza vigezo vya tenda hiyo kuleta majenereta ya umeme. Hii ina maana siyo Wizara ya Nishati na Madini, wala siyo Ofisi ya Waziri Mkuu, wala Ikulu waliokuwa na nguvu ya kuingilia mchakato wa tenda kwenye shirika hilo.

Swali: Kwa hiyo sheria inawapa nguvu hizo. Unataka kusema kuwa hakuna mtu au afisa nje ya sheria anayeweza kuingilia kati kama alivyofanya Waziri Mkuu?

Jibu: Hakuna. Sheria hiyo hiyo inaweka wazi kabisa kwenye ibara ya 38 kuwa vyombo vyote vinavyohusika na masuala ya tenda vitafanya kazi yake kwa “uhuru”. Hii ni katika kuzuia kile kilichofanywa na Waziri Mkuu katika suala la Richmond na Rais Kikwete kwenye suala la Dowans.

Swali: Lakini wapo wanaosema kuwa kutokana na dharura ya wakati ule hakukuwa na jinsi isipokuwa Waziri Mkuu kuingilia kati kuokoa jahazi. Unasemaje?

Jibu: Hili ni jibu ambalo nimelisikia kwa muda sasa. Kwamba “dharura” ile ilimpa nguvu Waziri Mkuu kuingilia utaratibu wa tenda. Kwamba, kutokana na hali hiyo basi sheria ya Manunuzi ya Umma ilisimamishwa kwa muda na hivyo kukatazwa kufanya kazi na kumpa Waziri Mkuu kuongoza mchakato wa kuipata Richmond. Mawazo hayo yana makosa.

Sheria ya Manunuzi ya Umma haijawasi kusitishwa na haijafutwa na hakuna afisa yoyote wa serikali akiwemo Rais anayeweza kuisimamisha kiholela au kwa kisingizio cha “dharura”. Zaidi ya yote,

Zaidi ya yote, sheria hiyo ilitarajia kuwa kuna wakati ambapo huduma au bidhaa fulani inahitajika kwa haraka na hivyo utaratibu wa kawaida wa utoaji wa tenda kutotumika. Ni kwa sababu hiyo ibara ya 59(2) ya sheria hiyo imeweka wazi kuwa endapo inatokea kuwa bidhaa au huduma inahitajika wakati wa dharura basi utaratibu wa haraka upatikanaji wa tenda waweza kutumika kwa kuzingatia kanuni kubwa mbili; kwanza, mazingira yaliyosababisha dharura hiyo hayakuweza kutarajiwa au kutokana na makosa ya bodi yenyewe kuchelewa na pili bodi itaweka nyaraka za kuelezea kwanini inatumia utaratibu huo wa haraka. Hivyo, Bodi ya Tenda ya Tanesco ilikuwa na nguvu zote za kufanya kazi hiyo.

Swali: Kwa mujibu wa mojawapo ya barua tulizosizoma kwenye magazeti mbalimbali Mhe. Lowassa aliona kuwa kule Tanesco wameshindwa kazi hiyo na ndiyo sababu ya yeye kuunda timu ya majadiliano na kuchukua madaraka ya kusimamia tenda. Unasemaje kuhusu hilo?

Jibu: Kama nilivyosema awali, Waziri Mkuu hana mamlaka ya kisheria ya kuingilia mchakato wa bodi ya tenda mahali popote; lakini la pili ni kuwa endapo kulikuwa na matatizo katika bodi ya tenda ya mahali fulani basi Mtendaji Mkuu wa Mamlaka ya Manunuzi ana uwezo wa kisheria kuingilia kati na siyo Waziri Mkuu. Hivyo, kwa kimsingi ni kuwa Waziri Mkuu alivunja sheria na hiyo peke yake ilikuwa ni sababu tosha ya kujiuzulu.

Swali: Lakini inaonekana alikuwa na nia njema ndio maana alichukua maamuzi hayo, ama sivyo?

Jibu: Yawezekana alikuwa na nia njema. Hata hivyo alipokula kiapo chake cha Ofisi ya Waziri Mkuu hakula kiapo cha “kulinda, kutetea na kuhifadhi” nia yake njema. Waziri Mkuu wetu kama walivyo watumishi wengine wakuu wanakula kiapo cha kuilinda na kuitetea Katiba ya Jamhuri ya Muungano na kiapo kingine cha utii kwa Rais aliyemteua na vile vile kile cha Usiri kama mshiriki wa Baraza la Mawaziri. Hivyo, nia yake njema haikumzuia kuwajibika au kujiwajibisha yeye mwenyewe.

Swali: Unachosema kinakubaliana kwa kiasi na kile kilichopo kwenye ripoti ya Mwakyembe. Umechota humo?

Jibu: La hasha; mtu yeyote anayeweza kutumia dakika chache kufikiri anaweza kufikia hitimisho ambalo nimelifikia mimi au walilofikia kina Mwakyembe. Wao walielezea hilo kwa maneno yafuatayo katika ripoti yao ile ya Kihistoria: “PPRA ilifanya uchunguzi makini na wa kina kujua kama Sheria na Kanuni za Ununuzi wa Umma zilifuatwa. Taarifa hiyo imebainisha wazi kuwa pamoja na nia nzuri ya Serikali ya kutaka kuiokoa nchi kutokana na hali mbaya ya umeme, mchakato mzima wa zabuni ulikiuka Sheria ya Ununuzi wa Umma ya Mwaka 2004 na Kanuni za Ununuzi wa Umma za Mwaka 2005”. Na vile vile kuwa “Kama vile Wizara hiyo haihusiki kabisa na utawala wa sheria na utawala bora, ikailazimisha TANESCO isiheshimu ushauri wa kitaalamu wa Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA) na kuingilia mchakato wa zabuni wa procurement entity nyingine kwa kuiweka pembeni Bodi ya Zabuni ya TANESCO, kuiagiza TANESCO ivunje sheria kwa kuwabadilisha wajumbe wa Bodi yake ya Zabuni na Wizara kufanya maamuzi ya ununuzi kwa niaba ya TANESCO na kuu
lazimisha uongozi wake kusaini mkataba na kampuni ambayo TANESCO waliikataa mara tatu kwa vigezo vya kitaalamu kuwa haifai kwa kazi hiyo. Huo ulikuwa udhalilishaji mkubwa wa viongozi na watendaji ndani ya TANESCO.”

Swali: Utawaambia nini wale wanaomini kuwa Waziri Mkuu ana uwezo wa kuingilia kati suala kama hilo wakati wa dharura? Kwamba wakati wa dharura serikali inaweza kufanya jambo lolote bila ya kujali sheria iliyopo?

Jibu: Wazo hilo liko miongoni mwa watu wetu wengi na wengine ni wasomi mahiri Binafsi ningeiadhibu bodi ya tenda ya Tanesco kwa kukubali kuingiliwa kati na Ofisi ya Waziri Mkuu. Ninaamini kama wangeenda mahakamani wangeweza kumzuia Waziri Mkuu kuendesha mchakato wa tenda nje ya ule uliopo kwenye sheria ya 2004 ma Kanuni zake za 2005. Nina uhakika wa asilimia 101 wangeshinda.

Lakini vile vile, Waziri Mkuu hana uwezo wa kutangaza dharura inayoweza kusababisha baadhi ya sheria kutokutumika na maagizo yake yakatosha kuwa sheria. Kwa sheria zetu sisi ni Rais tu anayo madaraka ya kutangaza dharua na hali ya hatari.

Swali: Tafadhali fafanua hilo.

Jibu: Bila ya shaka. Mojawapo ya sheria ambazo wengi wetu hatujawahi kuzisikia au kuona zikitumika ni ile ya Mamlaka ya Rais wakati wa Dharura (Emergency Powers) ya mwaka 1986. Sheria hiyo inampa Rais madaraka ya kuweza kutangaza hali ya hatari kwa nchi nzima au sehemu yoyote ya Tanzania Bara au Visiwani. Na hali ya hatari (dharura) hapa kwa mujibu wa sheria ni pamoja na masuala ya “vita, uvamizi, uasi, kuvunjika kwa amani, vurumai au jangana jingine lolote au maafa mengine” yawe yamesababishwa na asili au vinginevyo na ambayo yanatosha kufanya kuwa nia suala kitaifa. Ninaamini janga la umeme la 2006 na hata la mwaka huu yanaweza kutosha kabisa kutangaza hali ya dharura.

Sasa, Rais ndiye mtu pekee ambaye anaweza kutangaza hali hiyo na ndiye pekee anayeweza kutoa mamlaka yake hayo kwa mtu mwingine kwa mujibu wa sheria. Na ikimbidi kufanya hivyo basi hilo linatangazwa kwenye Gazeti la Serikali na siyo kwa simu au kwa mdomo tu ni lazima iwe kwa maandishi.

Swali: Sasa, yawezekana Waziri Mkuu alipewa madaraka hayo ya Rais na hivyo kupewa uwezo huo wa kwenda nje ya sheria ya Manunuzi?

Jibu: Ndiyo inawezekana. Lakini hadi hivi sasa hakuna mahali hata pamoja ambapo Taifa lilitangaziwa kuwa Rais ametangaza hali ya dharura. Na kama ilitangazwa, ilitangazwa katika toleo gani la Gazeti la Serikali? Nitakuwa tayari kusahihishwa endapo litatolewa tangazo la Rais kumpatia Waziri Mkuu au mtu mwingine yoyote madaraka hayo.

Swali: Kama Waziri Mkuu hakupewa madaraka hayo yeye aliyapata wapi?

Jibu: Hilo ndilo swali la karne. Ninachoona nikuwa “dharura” tunayoisema ni dharura kwa maana ya kawaida ya jambo lenye uhitaji uangalizi wa haraka na siyo kwa maana ya kisheria. Kwa sababu hiyo basi Waziri Mkuu hakuwa na uwezo wa kufanya hivyo.

Swali: Vipi kuhusu kwa kutumia sheria ya Kusimamia Majanga ambayo iko chini ya Wizara yake?

Jibu: Hata kwa sheria hiyo Waziri Mkuu hana uwezo wa kuingilia tenda ya chombo chochote kile. Sheria ile nayo imeweka utaratibu wa kufuata wa kushughulikia majanga mbalimbali na nani anaongoza na vyombo hivyo vinaratibiwaje.

Swali: Kama nimekuelewa vizuri ni kuwa Waziri Mkuu alifanya makosa kuingilia mchakato wa tenda ya Richmond na ilimtosha kujiuzulu?

Jibu: Sawasawa.

Swali: Vipi kuhusu madai ya kuwa Kamati Teule haikumtendea haki Waziri Mkuu na kumnyima haki yake ya asili ya kujitetea?

Jibu: Hilo nalo limekuwa hoja kubwa sana kwa watu mbalimbali kiasi kwamba kuna watu wasomi wanaamini kabisa kuwa Lowassa hakutendewa haki na kuwa alionewa na kina Mwakyembe. Sasa mimi sizungumzi kwa niaba ya Kamati Teule (sina uwezo, nguvu, wala sababu hiyo). Ninachoangalia ni vitu vichache.

Kwanza ni kuwa Kamati Teule ilisema wazi kuwa “Watu pekee waliokuwa wanaujua ukweli wenyewe, ukweli ambao ungeipa Kamati Teule msingi wa kumhoji Waziri Mkuu kwa kiapo, walikuwa watatu: Waziri Dk. Msabaha (Mb), Katibu Mkuu Mwakapugi na Mwenyekiti wa Bodi Balozi Kazaura.” Na kuwa watu hao watatu walikataa “katakata kupokea maagizo toka kwa Waziri Mkuu” kuipendelea Richmond. Lakini hata hivyo, baada ya kushindwa kufanya hivyo nje ya kiapo watu hao hao waliidokeza kamati hiyo kuwa ni kweli walipata maagizo hayo!

Ni kutokana na hilo Kamati hiyo iliidai kuwa “Pamoja na woga uliokuwa dhahiri wa watumishi hao, ushahidi wa maandishi, wa mdomo na kimazingira ambao Kamati Teule iliupata kutoka kwa mashahidi mbalimbali, unamhusisha Waziri Mkuu na mchakato wa maamuzi katika suala hili la Richmond.”

Ni kutokana na hilo, Kamati Teule ilipofika wakati wa kutoa mapendekezo yake ilimpa nafasi Waziri Mkuu kukanusha, kupinga, kukataa, kujitetea au kujibu hoja zilizotolewa. Pendekezo lao kuhusu Waziri Mkuu lilisema hivi “Kwa kuzingatia umuhimu wa nafasi aliyonayo Mhe. Waziri Mkuu katika uendeshaji wa shughuli za Serikali na uongozi wa nchi kwa ujumla, ni wajibu wake yeye mwenyewe kupima uzito wa matokeo ya uchunguzi huu na wajibu wake kikatiba ndani na nje ya Bunge. Vile vile ni wajibu wa Bunge ambalo linathibitisha uteuzi wake kwa mujibu wa Ibara ya 51 inayothibitisha uteuzi wake. Kuangalia ikiwa matokeo ya uchunguzi huu hayajaathiri hadhi na uzito wake ndani ya Bunge.”

Kamati Teule haikuitisha kujiuzulu kwa Lowassa. Ilimpa nafasi ya “kupima uzito” wa matokeo ya huo uchunguzi na kwa Bunge kupima “kuangalia” kama matokeo ya uchunguzi hayajaathiri hadhi na uzito wake Bungeni”.

Swali: Hebu vunja vunja hapa nielewe naona kizunguzungu kwa kweli!

Jibu: Bila ya shaka. Kamati ya Mwakyembe ilimfungulia mwanya Lowassa kujibu hoja zao hapo hapo Bungeni. Hata kama hakuweza kuitwa kwenye Kamati (kwani hakuna mtu aliyemtaja moja kwa moja chini ya kiapo) kwa vile Kamati ya Bunge ina nguvu za Bunge na Bunge bado linaweza kusikiliza jambo linalotoka kwenye Kamati Lowassa angeweza kufanya mambo kadhaa.

Kutoa hoja mjadala uhairishwe ili apate nafasi ya kuandaa majibu yake. Hili naamini ndilo alilotakiwa kufanya. Angeweza kutoa hoja asubuhi hili kuwa “baada ya kupima uzito” wa ripoti ya Kamati Teule anamuomba Spika mjadala uahirishwe japo kwa siku moja ili aweze kupitia vielelezo mbalimbali na kuandaa majibu yake. Hakufanya hivyo.

Kama tayari alikuwa anajua msimamo wake angeweza asubuhi ile kuanza kupangua hoja moja baada ya nyingine, kuanzia barua zinazodaiwa kutoka kwake kwenda maafisa mbalimbali wa Wizara na za kutoka kwao kwenda kwake. Angeonesha kuwa hakufunja sheria yoyote na angeweza kutetea madaraka yake ya kuingilia utaratibu wa tenda na aliyapata wapi. Hapa angeweza kuonesha tamko la Rais kutoka sheria ya Madaraka ya Dharura kuwa Rais alimpa uwezo huo kwa agizo namba fulani lililotolewa kwenye gazeti la serikali toleo fulani. Hakufanya hivyo.

Angeweza kuomba Bunge liahirishwe ili aweze kufanya mazungumzo na Rais (aliyekuwa tayari Dodoma wakati ule) ili aweze kumueleza upande wake na kupata msimamo wake na kumtaka asimame upande wake atakapojitetea Bungeni. Hakufanya hivyo.

Angeweza kujiuzulu bila ya kujitetea. Hilo alilifanya.

Lowassa aliamua kutumia njia nyepesi zaidi ya kujiuzulu bila ya kujitetea.

Swali: Sasa alidai kuwa “natural justice” sijui haikufanyika kwake. Wewe hulioni hilo?

Jibu: Kwa mtu mwingine anaweza akaliona hivyo siyo mimi. Haki ya msingi ya asili (natural law) haimaanishi mtu kupewa nafasi ya kujitetea kwenye nafasi moja au sehemu moja tu. Haki ya kujitetea inaponyimwa ni pale mtu anapoadhibiwa pasipo kusikilizwa kabisa (condemnation without hearing). Yaani, mtu anaambiwa “wewe umeiba mbuzi” na kabla hajafungua mdogo wake anapigwa risasi! Lowassa hakunyimwa haki ya kujitetea!

Lowassa alipewa nafasi ya kujitetea, na akaamu kutoitumia na badala yake aliitumia kukandia Kamati Teule na kudai kuwa walichokuwa wanakitaka ni “Uwaziri Mkuu” na kuwa atawapa takwa hilo. Hakutaka kujitetea. Lowassa alipewa nafasi ya natural justice kuelezea upande wake mbele ya Bunge, hakufanya hivyo.

Kwa msingi huo, hoja ya kuwa Lowassa alionewa kuwa hakusikilizwa haina msingi isipokuwa kwa watu ambao hawataki kukumbuka kilichotokea siku ile. Lowassa angeweza kujitetea vizuri kabisa siku ile, angeweza kupangua kila hoja iliyotajwa dhidi yake, angeweza kuhutubia kutwa nzima Bungeni na kuonesha mapungufu kiasi cha kusababisha Bunge kupiga kura ya kukataa ripoti ya Mwakyembe; hakufanya hivyo! Aliamua kuzira kujitetea.

Swali: Ina maana basi ni yeye pekee ndiye anabeba lawama za kujiuzulu kwake na siyo Bunge, Spika au kina Mwakyembe!

Jibu: Naam! Na ninaamini hata kabla ya Kamati kutoa ripoti yake Lowassa alitakiwa awe amekwisha jiuzulu endapo mapendekezo yake ya baadaye kuhusu Richmond yalipokataliwa na Rais.

Swali: Hilo jipya! Unasema kuna mapendekezo ambayo yalikataliwa na Rais?

Jibu: Ndiyo. Katika makala mbalimbali unazosisoma magazetini utaona mawasiliano kati ya Waziri Mkuu, Ofisi yake na Wizara. Hata hivyo hujaona mawasiliano ya Waziri Mkuu na Rais au Ikulu. Mawasiliano hayo ndiyo ungekuuwa utetezi mkubwa wa Lowassa dhidi ya tuhuma dhidi yake. Kwa vile alishindwa kumshawishi Rais kufuta huo Mkataba kama alivyofanya yale ya Dawasa, basi kuendelea kusimamia kitu ambacho yeye mwenyewe alikuwa hakubaliani nacho kunatosha kumfanya ajiuzulu. Angemwandikia mapema zaidi Rais kuwa kutokana na unyeti wa suala hilo na kwa vile kwa moyo safi na dhamira njema asingeweza kusimamia suala la Richmond basi angeomba aondolewe madarakani au yeye mwenye kujiuzulu. Hilo lingemfanya shujaa.

Kwa kukubali kusimamia kitu ambacho hakukiamini ili tu mambo yaendee ni sifa mbaya ya kiongozi na ninaamini kabisa kuwa ingetosha kuwa sababu nyingine ya kujiuzulu. Tanzania inahitaji viongozi ambao wako tayari kuwajibika kwa makosa yao na kuwajibika vile vile pale inapobidi kwa makosa ya wengine ili kulinda usafi wao. Lowassa hakufanya lolote kati ya hayo mawili.


Yona Fares Maro
I.T. Specialist and Digital Security Consultant

– – –
Subject: LOWASSA ALICHELEWA KUJIUZURU

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *