CCM YAAGIZA MAGARI 200 KWA AJILI YA UCHAGUZI 2010

LENGAI OLDOINYO

Wakati Watanzania wengi hawana nyumba za kudumu, Hawana Madawati ya shule, Hawana Zahanati za matibabu, Hawana barabara za kuwafikisha makwao wakati wa mvua, Hawana chakula kwa ajili ya ukame uliotishia Taifa. CCM wameagiza magari 200 ya kifahari kwa kodi za wananchi kwa ajili ya uchaguzi wa 2010.

Wakati huo huo inasadikiwa wameshirikiana na TRA ili kukwepa kodi pindi magari hayo yatakapokuwa yanaingizwa nchini. Watanzania tunashindwa kuelewa kuwa chama cha CCM kiko madarakani kuwanyinya Watanzania au kiko madarakani iuwasaidia Watanzania. Kila mahali kunanuka uvundo.

Wakati nusu ya Mawaziri wake wakiwa na kesi za kula rushwa, kugushi vyeti, kufanya biashara wakiwa viongozi, kununua mashirika na nyumba za shirika la nyumba kwa hila, Ufisadi, ubadhirifu wa mali za umma bado wanaongeza maajabu mengine ndani ya chama bila kujali kuwa wanaowaongoza ni watu masikini hohe hahe.

Chama cha mapinduzi miaka yake yote kilipokaa madarakani wanawaza kuweka nguvu zao zote za kiutawala katika uchaguzi. Wakishaingia madarakani ni ufisadi tu unaendelea. Hivi Watanzania lini tutapata unafuu wa maisha.

Akihutubia kwenye kampeni ya operesheni Sangara maeneo ya vijijini mkoani Tanga, Dk Slaa alisema Chadema haiwezi kuvumilia dhambi hiyo na kwamba itawasha moto katika bunge lijalo.

“Mimi na chama changu tutafuatilia kuhakikisha wanalipa kwa sababu kodi ni lazima kwa kila mtu,” alisema Dk Slaa ambaye ni mbunge wa Karatu. “Hii ni hujuma isiyopaswa kuvumiliwa na iwapo watashikilia msimamo wa kukwepa kodi hiyo, bunge lijalo hakutakalika.”

Katibu wa Itikadi na Uenezi, Kapteni John Chiligati alikiri CCM kuagiza magari ya uchaguzi, lakini akagoma na kukanusha wala hataki kukubali kwamba imekwepa kodi. CCM haitaki kuingia katika malumbano yasiyo ya lazima na vyama vya upinzani na kuwataka Watanzania wanaotaka ukweli juu ya suala hilo, kuwasiliana na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kwa ufafanuzi. Ninachoamini mimi ni kuwa TRA iko chini ya Serekali inayoongozwa na CCM hivyo hapatakuwepo na ukweli. Tunaviomba vyama vya siasa viombe wahasibu kutoa Jumuiya za kimataifa kuanza kukichunguza Chama tawala CCM

Alisema ni kweli CCM imeagiza magari kwa ajili ya maandalizi ya uchaguzi na kwamba imefanya hivyo baada ya kuona sasa imebakia miezi tisa tu kabla ya uchaguzi huo. Alisisitiza kuwa suala la CCM kununua magari halijaanza leo wala jana kwa kuwa wamekuwa wakifanya hivyo mara nyingi hasa kwa kuzingatia ni chama kikubwa, chenye uwezo wa kifedha na majukumu mengi kwa ajili ya taifa na watu wake.

“Hatuna muda wa malumbano na vyama vya upinzani… tuna miezi tisa tu kuingia kwenye uchaguzi. Lakini ufahamu pia kuwa sisi ni chama kikubwa. Suala la kununua magari hatujaanza leo wala jana. Tumekuwa tukifanya hivyo mara nyingi tu,” alisema Chiligati.

Huwa najiuliza katika maisha ya Watanzania kipi kina umuhimu zaidi kununua madawa ya watu wanaokufa kwa Malaria kila siku, Kununua madawati ya watoto wa shule, kuwajengea alibino makazi ya kudumu, kujenga viwanda na kufufua mashirika ya umma watu wapate ajira au kukipigia chapuo chama cha CCM kishinde uchaguzi. Kati ya haya yote niliyoyataja na kununua magari ya kifahari kwa ajili ya uchaguzi kipi chenye umuhimu. Shirika la ndege linaloweza kwenda nje na kuja na watalii limekufa CCM hawalioni hilo. Shirika la reli linalopeleka watanzania kanda ya Ziwa na kuja na bidhaa zinazozalishwa kule hawalioni.

Barabara za Kigoma watu wanalala njiani na watoto wadogo kipindi cha nvua hawazioni wao wanaona la muhimu ni kuleta magari ya uchaguzi. Kweli penye miti hapana wajenzi.

8 thoughts on “CCM YAAGIZA MAGARI 200 KWA AJILI YA UCHAGUZI 2010

  1. Ayoub Kafyulilo

    Inasikitisha!
    Mwaka 2005, waliagiza magari zaidi ya hayo kwa ajili ya kamapeni, sasa yale yote yamekwenda wapi hadi wanataka mengine tena? Mbona uchaguzi unatumia gharama nyingi na kubwa za kutisha kuliko kiasi kinachowekezwe katika kujenga hospitali na mambo mengine yanayogusa maisha ya masikini? tuna yatima wangapi ambao wameshindwa kabisa hata kwenda shule kwa kukosa ada, kwanini CCM isitoe kidogo japo kuchangia kwenye hilo?

    Mimi nina wazo kwamba vyama vya siasa visipewe Ruzuku. Vijiendeshe! serikali inashindwa kutoa hela kwa ajili ya kuendeshea mashirika ya umma, kama vile shirika la reli, inashindwa kuwekeza kwenye afya na usalama wa watu, inawekeza zaidi kwenye vyama. Kwanini vyama visijiendeshe kama ambavyo serikali imekuwa ikisisitiza taasisi nyingine zijiendeshe? Ruzuku ambayo vyama vinapewa ndiyo inayotoa mwanya kwa vyama vya siasa kuiba fedha ya serikali kwa kisingizio cha Ruzuku. CCM hawawezi kutuambia kwamba hiyo yote ni hela ya Ruzuku tu, na bado wanahitaji hela nyingine ya kununulia Tshirt za kutuhonga, plus pesa za kununulia kura. Hiyo hela yote wametoa wapi kama siyo wamefisadi kitu kingine tena? Nina wasiwasi kuna EPA nyingine imezaliwa hapa.

    Kwa mtazamo wangu, vyama vya siasa vinapata ada ya wanachama ya kila mwaka, wana miradi mbalimbali, wanapta misaada kutoka mashirika mbalimbali ya kimataifa, wafanyabiashara nk. Kuna sababu gani ya serikali kutumia fedha nyingi kutoa ruzuku kwenye vyama ambapo matumizi yake ni hayo ya kununua magari hata kama wanayo? Tuna matatizo mangapi nchini, ingekuwa vipi kama magari hayo yangekuwa ni ambulance ya kila hospitali ya wilaya? CCM imeshindwa kutekeleza kauli mbiu yake ya maisha bora kwa kila mtanzania, badala yake inawekeza kwenye kampeni tena? Mwakani watatuambia kila mtanzania atapewa gari lake na nyumba yake, bado tutawakubali, halafu wakipewa nchi watanunua ndege za kampeni. Inaumiza sana unapoona, mliowapa dhamana ya maisha yenu, wanawakebehi na kuwaona ni wehu.

    Naogopa kusema kwamba thamani ya maisha ya Mtanzania masikini wa kijijnini imekuwa ndogo kuliko hata wakati wa ukoloni. Huwezi kabisa kutarajia kwamba watanzania wenzetu wanaojua hali zetu za maisha wanaamua kutumia kiasi kikubwa hivyo cha pesa kununua magari kwa ajili ya kampeni (kwa ajili ya kutudanganya tuwepe tena ulaji).

  2. Amani Kerege

    Ooh, hii ni kufuru! Inawezekanaje kuwa na chama kikubwa katika nchi maskini? Wanafunzi wanakosa mikopo eti serikali haina fedha lakini chama kinaweza kuagiza magari yote haya wapite mitaani wakituringia. Watu hawana maji safi na salama ya kunywa wengine wanawaza starehe zao tu. Vijana hawana kazi kwa kuwa viwanda vimekufa wenzetu wanawaza uchaguzi tu. Wanafunzi wetu primary schools wanafeli kwa kukosa vifaa na kwa maslahi finyu kwa walimu, lakini watu wamefumba macho. Hivi tutapona kweli. Waswahili wanasema usile na kipofu ukamgusa mkono!! (Maana unakula upande wake nae maskini haoni lakini ukinogewa hujali hata kumuonyesha kwamba mikono yako inakwenda upande wake).

    Kwa hiyo haya ndiyo maisha bora tuliyoahidiwa 2005? Hivi Mtanzania wa kawaida hayaoni haya?

  3. jovias mwesiga

    Jamani nchi inajengwa kwa mikakati, tutajuaje matatizo ya wanmachi kama hatuwafikii? mnataka tununue helkopita sie CHADEMA?

    Hali ya barabara zetu ni mbaya hivyo tunanunua magari haya ili tuweze kuwafikia wananchi tujue matatizo yao na baada ya uchaguzi tujue tunayatatua vipi, tueleweni jamani ni katika kuwatumikia.

  4. wrlmakundi

    Nonsense! Kwani hakuna viongozi na wanachama vijijini, jimboni, wilayani? Wanaishi hapo siku zote wanajua matatizo YAO!!

  5. Niocodemus Eatlawe

    Mnauliza maswali mazuri kweli ila hayana majibu ya kiutendaji. It is matter of power and control. Who has power and control of resources? They have. Citizens end up getting makombe ya pilau, kofia, kanga, pombe (ulanzi au busa kule kwetu), tishirts na lifti za wakati wa uchaguzi! Wakishapata kula (siyo kura maana kura unayo wewe) wanageuka kuwa wasaliti wa wapiga kura!

    Hizi siasa za dunia ya tatu ni geresha tupu na demokrasia ni kiinimacho cha kudangaya mazezeta! Sorry for pejorative word! I am very disappointed by what politicians do. Wait for our time to come! Kama makaburu waliachia ngazi na nguvu zao zote itakuwa kwetu! Ni swala muda tu. Wanasema huwezi kudanganya watu wote wakati wote! Hata mjinga iko siku atashtuka. That day is coming! But as for now let them engulf and grab whatever they can but finally it come out through their noses!

  6. LENGAI OLDOINYO

    Ndugu Nico,
    Mimi nimesikitika sana jana nyumba moja kule Dodoma imeungua moto na kwisha kabisa lakini wakora wa CCM wanaagiza magari ya uchaguzi badala ya kuagiza magari ya zima moto na wagonjwa. Kweli CCM wameamua Tanzania iwe kisiwa chao cha kukinyonya maisha. Hivi Watanzania mko au mmelala usingizi. Amkeni kumekucha. Mimi nina imani kama za kwako. Kama Sadam alishitakiwa bila makosa hata JK iko siku atapandishwa kizimbani. Ukiwa kiongozi jiandae kupanda karandinga once unapoboronga. Mzee Mwinyi kula kuku mzee. Wacha wajichongee wenyewe ila kitanzi kinawangoja. Milosovic alishirikiana na Mawaziri wake kuboronga katika utawala wake lakini kizimbani alipanda mwenyewe.

  7. Shirly Wang

    Binzhou Group Co, Ltd ni kampuni ya kundi ziko katika mji Binzhou, mkoani Shandong China.
    Tuna kila aina ya bidhaa mbalimbali kama vile vya nguo wax halisi, soso super, London wax, nk
    Kutegemea ubora kamilifu, tuna biashara kuanzisha uhusiano na zaidi ya 35 nchi na kanda, kama vile Marekani, Afrika, Canada, Uingereza, Australia, Japan,
    Asia ya Kusini, Korea, Mashariki ya Kati, nk Kila mwezi sisi kuzalisha na kuuza nje zaidi ya 55
    vyombo vya miguu 20 kwa Afrika.
    Sisi ni katika juhudi za kukuza biashara zetu kwa wateja wote wa dhati kutoka nje ya nchi, tafadhali kujisikia huru kuwasiliana nasi kwa maelezo zaidi, tunatarajia kufikia kuheshimiana pamoja faida yetu
    baadaye kwa ushirikiano wetu kwa moyo mkunjufu.
    —————-
    Shirly Wang
    Binzhou Group Co.,Ltd
    Add: No.359, Huanghe 6 road, Binzhou, Shandong, China
    Email : sales3@bzh.net.cn
    Website: http://www.bzh.net.cn
    Tel:86-543-388 8282
    Fax:86-543-316 5790

  8. LENGAI LETIPIPI

    Haya sasa kumezuka jipya. Wameshaingia madarakani umeme umekuwa wa mgao na Tanesco wanadaiwa Bilioni 180. Watanzania lazima tujue kudai haki zetu. Pesa ya magari mia mbili ingeweza kuweka miundo mbinu mizuri ya umeme.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *